BoT Kuanzisha Kampuni Maalum ya Udhamini wa Mikopo Kuwainua Wajasiriamali - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, December 9, 2025

BoT Kuanzisha Kampuni Maalum ya Udhamini wa Mikopo Kuwainua Wajasiriamali


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Serikali kupitia Benki Kuu imepanga kuanzisha kampuni ya udhamini wa mikopo (Credit Guarantee Public Limited Company) yenye lengo la kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kukua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Gavana Tutuba alitoa kauli hiyo leo, Desemba 8, wakati wa kikao chake na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za fedha kilichofanyika katika Ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa huduma za udhamini wa mikopo zimeendelea kupanuka katika mataifa mbalimbali, akitolea mfano nchi ya Malaysia ambayo imeendesha kampuni ya udhamini wa mikopo kwa zaidi ya miaka 50.

Hatua hii inatarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati, kuongeza ajira, kupanua wigo wa mapato ya serikali kupitia kodi, na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi kwa kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali. Zaidi ya hapo, kuanzishwa kwa kampuni ya udhamini wa mikopo kutachochea maendeleo ya maeneo mapya ya uwekezaji, hatua ambayo itaboresha ushindani wa taifa katika uchumi wa kisasa.

Akizungumza kwa niaba ya benki za biashara, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Bw. Theobald Nsabi, amepongeza mpango huo na kusisitiza utayari wa benki hizo kushirikiana na Serikali katika kuanzisha kampuni hiyo pamoja na kuendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za kukuza sekta ya fedha.

Kwa sasa, huduma za udhamini wa mikopo nchini zinatekelezwa na Serikali kupitia Mifuko miwili ya Udhamini wa Mikopo inayosimamiwa na BoT ambayo ni Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS).

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na viongozi kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam(DSE).



No comments:

Post a Comment