
Benki Kuu ya Tanzania kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza Dhamana za Serikali za muda mrefu (Hati fungani) na dhamana za Serikali za muda mfupi (“Treasury bills”) ikiwa ni njia ya Serikali kukopa fedha kutoka kwenye Soko lake la ndani ambapo mnunuzi anaweza kuwa taasisi, vikundi, benki, mtu binafsi n.k.
Dhamana Serikali za muda mrefu ni zile ambazo muda wake wa kuiva unazidi mwaka mmoja. Dhamana hizi huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani na njia isiyo ya ushindani kupitia minada inayoendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania na baada ya hapo uuzaji wa dhamana za Serikali huuzwa kwenye upili yaani Soko la hisa la Dar es Salaam.
Mwekezaji atanunua Hati fungani kupitia kwa Mawakala ambao ni benki zote za biashara zilizosajiliwa na kupatiwa leseni ya biashara na benki na Benki Kuu ya Tanzania au Mawakala wa soko la Hisa la Dar-es- Salaam waliopatiwa leseni na kusimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.
Kiwango cha kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali za muda mrefu (Hatifungani) ni kuanzia kiwango cha shilingi 1,000,000.00.
Ili uweze kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali , ni lazima kufungua akaunti maalum ya uwekezaji inayoitwa “Central Depository System Account” – (CDS). Akaunti hii ni tofauti na akaunti ya akiba kwa kuwa inatumika kutunza kumbukumbu na taarifa zote za uwekezaji.
Kufungua akaunti hii hakuna gharama yoyote, na mwekezaji atatakiwa kuwasilisha nyaraka za utambulisho kama vile kitambulisho cha taifa (NIDA), namba ya mlipa kodi (TIN), pamoja na picha mbili ndogo za pasipoti.
Wawekezaji wa dhamana za Serikali za muda mrefu hupata malipo ya faida (coupon) mara mbili kwa mwaka, na Benki Kuu ya Tanzania hulipa coupon moja kwa moja kupitia akaunti za benki kama zilivyoainishwa nakila mwekezaji.

No comments:
Post a Comment