Maryprisca Atoa Wito wa Ushirikiano Kuboresha Malezi ya Watoto - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, December 12, 2025

Maryprisca Atoa Wito wa Ushirikiano Kuboresha Malezi ya Watoto



Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii kwa ujumla kuendeleza ushirikiano na Serikali katika kuhakikisha watoto waliopo kwenye makao wanapata fursa sawa za malezi na maendeleo kama watoto wengine wote nchini.

“Niwaombe mashirika na wadau mbalimbali muendelee kuiunga mkono Serikali katika kuimarisha huduma katika makazi ya watoto ili wasiishi kwa kujiona duni. Ninyi ni watu muhimu, mnapendwa na Taifa linawahitaji. Msikate tamaa; someni kwa bidii, zingatieni maadili, muwe na nidhamu na tumieni fursa mnazopata ili kufikia ndoto zenu,” amesema Mhe. Maryprisca.

Amesema hayo wakati wa ziara yake katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo jijini Dodoma, alipotembelea miradi, kuangalia miundombinu na kupokea taarifa ya maendeleo ya huduma zinazotolewa na makao hayo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Maryprisca amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha ustawi wa jamii na mifumo ya ulinzi wa mtoto, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za malezi mbadala na usimamizi wa Makao ya Watoto nchini ili yaweze kutoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.

“Nimefurahishwa kuona jitihada kubwa zinazofanywa katika kutoa huduma za elimu, afya, lishe, ushauri nasaha na malezi. Wizara itaendelea kuwezesha Makao haya ili yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” ameongeza.

Aidha, ameupongeza uongozi wa Makao ya Taifa ya Kikombo kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka waendeleze ushirikiano na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha kila mtoto analelewa katika mazingira salama, yenye upendo na yanayomjenga kimaadili.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Wakili Amon Mpanju, amesema watumishi wa Makao hayo wana weledi mkubwa na uwezo wa kutambua changamoto pamoja na mahitaji ya watoto wanaopokelewa katika makazi hayo.

“Hawa watumishi unaowaona hapa wana uwezo wa kukaa na watoto, kuzungumza nao kwa mbinu mbalimbali. Ndiyo maana nasema hawa si watu wa kawaida bali ni watu walioaminiwa na Serikali kutusaidia kukiendeleza kituo hiki,” amesema Mpanju.

Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Makao hayo, Afisa Ustawi wa Jamii, Anord Fyataga, amesema kituo kimefanikiwa kuimarisha huduma za ushauri nasaha, kuwaunganisha watoto 20 na familia zao, kuboresha ufaulu wa watoto wa shule ya msingi na sekondari kwa asilimia 2, pamoja na kuwajengea watoto 40 ujuzi wa stadi za maisha ikiwemo ushonaji wa nguo kwa kutumia cherehani.

Kwa ujumla, ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto na kuhakikisha makao yote nchini yanatoa huduma bora zinazowajengea watoto msingi imara wa elimu, afya, maadili na ustawi wa jumla.


CHANZO NI MJJWM
Dodoma







No comments:

Post a Comment