Na Anangisye Mwateba – Manyoni, Singida
Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kutekeleza Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyobora, mpango wenye lengo la kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la kaya na Taifa, kuongeza ajira pamoja na kuimarisha uhifadhi wa mazingira. Kupitia mpango huu, sekta ya ufugaji nyuki inatarajiwa kuwa miongoni mwa sekta kinara katika kuchangia fedha za kigeni, kutoa ajira kwa vijana na wanawake, na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika mafunzo ya ufugaji nyuki kwa vikundi vya wafugaji nyuki wilayani Manyoni mkoani Singida, Mratibu wa Kitaifa wa Mpango huo, Bi. Imelda Emmanuel, alisema mpango huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2025 hadi 2035, katika wilaya 52 zilizopo kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara. Kwa mwaka huu wa fedha, utekelezaji umeanza katika Halmashauri za Wilaya ya Manyoni na Singida (Mkoa wa Singida), pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Sikonge, Kaliua na Urambo (Mkoa wa Tabora).
Bi. Imelda alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa mpango huo, sekta ya nyuki inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa asali na mazao mengine ya nyuki, kupanua masoko ya asali nje ya nchi kutoka asilimia 5 hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2035, pamoja na kuongeza fursa za ajira kupitia shughuli za ufugaji nyuki.
Licha ya manufaa hayo, mpango huu pia umeainisha changamoto zinazokusudiwa kutatuliwa, ikiwemo uharibifu wa maeneo yanayofaa kwa ufugaji nyuki, matumizi ya mizinga ya magome, mwingiliano wa shughuli za ufugaji nyuki na shughuli nyingine za kibinadamu, uhaba wa rasilimali fedha na uwekezaji mdogo katika sekta.
Changamoto nyingine zinazolengwa kutatuliwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa tafiti za kisayansi zinazoweza kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali katika sekta ya ufugaji nyuki, huduma duni za ugani, upungufu wa takwimu sahihi na za wakati, sambamba na vikwazo vinavyoathiri biashara ya asali na mazao mengine ya nyuki.





No comments:
Post a Comment