
Na Angela Msimbira, OWM–TAMISEMI
Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) imewakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mpango Mkakati wa Ofisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2030/31, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika mamlaka za serikali za mitaa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika Desemba 19, 2025 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Profesa Tumaini Nagu, amesema kikao hicho ni sehemu ya mchakato mpana wa kuhakikisha Mpango Mkakati unaoandaliwa unazingatia uhalisia wa mahitaji ya jamii pamoja na mwelekeo wa kitaifa wa maendeleo.

Profesa Nagu amesema Serikali tayari imezindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inaendelea na maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo taasisi zote za umma, ikiwemo TAMISEMI, zinapaswa kuandaa mipango itakayochangia kikamilifu kufikia malengo hayo makubwa ya kitaifa.
Amefafanua kuwa kabla ya kuanza kuandaa Mpango Mkakati mpya, TAMISEMI ilifanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati unaomalizika muda wake mwezi Juni 2026, kwa kushirikisha Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na watendaji katika mamlaka za serikali za mitaa, vituo vya kutolea huduma za afya na shule.
“Kikao hiki ni mwendelezo wa vikao vingine vilivyotangulia, na lengo lake ni kupata maoni ya wadau kuhusu utekelezaji wa mpango unaomalizika pamoja na rasimu ya mpango unaoandaliwa, ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji kuboreshwa,” amesema Profesa Nagu.
Amesisitiza kuwa Serikali ina mtazamo wa kupanga na kutekeleza mipango kwa pamoja kwa kuweka malengo ya muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu, jambo linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi za umma, washirika wa maendeleo na wadau wengine muhimu.
Aidha, amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa ya kikao hicho kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru, akieleza kuwa maoni hayo yatasaidia kuandaa Mpango Mkakati utakaoweza kujibu changamoto zilizopo na kuakisi mahitaji halisi ya wananchi katika ngazi zote za serikali za mitaa.
Kwa upande wao, washiriki wa kikao hicho wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo wa OWM–TAMISEMI, wawakilishi wa wizara, taasisi za serikali na washirika wa maendeleo, wameeleza utayari wao kushiriki kikamilifu katika mchakato huo ili kuhakikisha Mpango Mkakati unaandaliwa unakuwa chombo madhubuti cha kuleta maendeleo endelevu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bw. John Cheyo, amesema lengo kuu la kikao hicho ni kujadili na kupokea maoni ya wadau kuhusu Mpango Mkakati wa OWM–TAMISEMI kwa kipindi cha 2026/27 hadi 2030/31, ili kuuimarisha zaidi kabla ya kuanza utekelezaji wake rasmi.




No comments:
Post a Comment