
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratias Ndejembi, amesema utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) unatarajiwa kuwanufaisha wananchi wa Tanzania kwa kiasi cha takribani dola za Marekani milioni 10 (USD 10M) kupitia shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) pindi mradi huo utakapoanza kutekelezwa.
Amesema, mbali na manufaa ya kijamii, mradi huo utaingizia taifa mapato mbalimbali yakiwemo kodi za zuio pamoja na kodi ya mapato ya kampuni, hatua itakayoongeza mchango wa sekta ya nishati katika uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa kikao na watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mtumba jijini Dodoma, Waziri Ndejembi amesema mradi huo utakaotekelezwa katika kijiji cha Likong’o mkoani Lindi ni wa kimkakati kwa maendeleo ya taifa.
Amehimiza kufuatwa kwa taratibu, sheria na miongozo iliyopo ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na rasilimali hiyo.
Ameongeza kuwa halmashauri katika maeneo yatakayotekelezwa mradi huo zitanufaika moja kwa moja kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo itakayoboreshwa kutokana na mapato yatokanayo na mradi huo.
Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, mradi wa LNG pia utafungua fursa kwa sekta nyingine za uzalishaji ikiwemo sekta ya madini pamoja na sekta nyingine muhimu za kiuchumi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi mapema kuhusu mradi wa gesi asilia na faida zake ili kujenga uelewa, kuondoa hofu na kuongeza uungwaji mkono wa jamii katika maeneo husika.
Kwa upande mwingine, Waziri Ndejembi amewataka wataalamu wa TPDC kuzingatia uzalendo, uwazi na kutanguliza maslahi mapana ya taifa katika utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (LNG), ili kuhakikisha manufaa ya rasilimali hiyo yanawanufaisha Watanzania kwa vizazi vya sasa na vijavyo.



No comments:
Post a Comment