Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imeanza mkakati wa ujenzi wa barabara za njia nne katika barabara kuu zitakazounganisha mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa pamoja na kupunguza ajali za barabarani.
Ulega amesema utekelezaji wa mpango huo unalenga kuimarisha sekta ya miundombinu nchini sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia usafirishaji wenye ufanisi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Waziri huyo ameyasema hayo leo Mei 10, 2026 jijini Dodoma wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa wanafunzi washindi wa shindano la andiko la ubunifu wa kupunguza msongamano wa magari mijini “Foleni Challenge 2026”.
Katika hafla hiyo, Ulega amesema Serikali imeamua kuwashirikisha vijana katika kutafuta suluhisho la changamoto za usafiri mijini kupitia ubunifu wao, ikiwa ni njia ya kuhamasisha matumizi ya maarifa ya darasani katika vitendo na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
“Tumewashirikisha vijana sio kwa sababu hatuna wataalamu, bali tunaamini vijana wana nafasi kubwa ya kushiriki katika ujenzi wa taifa lao. Tunataka mawazo yao, ubunifu wao na nguvu zao viwe sehemu ya maendeleo ya Tanzania,” amesema Ulega.
Amesema Tanzania ina wataalamu wa kutosha katika sekta ya miundombinu, hali inayodhihirishwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa ya SGR pamoja na Julius Nyerere Hydropower Project.
Aidha, Ulega amewataka vijana kuendelea kuipenda, kuiamini na kuilinda Tanzania huku akiwataka kupuuza wanaobeza mafanikio yanayofanywa na Serikali.
Amesema taifa linahitaji kizazi chenye uzalendo, maono na uthubutu wa kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo endelevu.
Pia amewahimiza vijana walioshiriki shindano hilo kutosita kufungua kampuni zao, akieleza kuwa Wizara ya Ujenzi ipo tayari kuwasaidia kupitia taasisi zake katika mchakato wa usajili ili waweze kutumia taaluma zao kujijengea uchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Ambapo mshindi wa kwanza wa shindano hilo ni Mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar wa Salaam (UDSM), Tukay Thomas,amepewa zawadi ya shilingi milioni 10, tuzo, kompyuta.
Awali, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Arch. Dkt. Daniel Matondo, alisema jumla ya maandiko bunifu 561 yalipokelewa, ambapo 328 yalikuwa ya wanafunzi na 233 hayakuwa na utambulisho. Maandishi hayo yalitoka katika vyuo 38 vya ndani na vyuo vinne vya nje ya nchi. Alisema kati ya maandiko hayo, 176 yalitimiza vigezo na kuingia katika hatua ya uchambuzi wa kina.
Kwa mujibu wa Dkt. Matondo, suluhisho zilizowasilishwa zilionyesha kuwa changamoto ya msongamano wa magari inaweza kutatuliwa kwa mbinu mbalimbali badala ya kutegemea njia moja pekee.
Alisema mapendekezo 19 yaliyoibuka yaligusa maeneo muhimu ya usafiri na mipango miji, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usafiri wa umma na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa trafiki.
Mapendekezo hayo pia yalijumuisha ukamilishaji wa mtandao wa mabasi yaendayo haraka (BRT), ujenzi wa flyover, utenganishaji wa barabara katika maeneo yenye msongamano mkubwa, pamoja na upanuzi wa miundombinu ya usafiri usiotumia magari.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuhamisha baadhi ya huduma nje ya maeneo ya biashara kuu, ujenzi wa barabara za haraka, kuongeza njia katika maeneo yenye msongamano mkubwa, kudhibiti magari makubwa mijini na kuboresha usafirishaji wa mizigo.
Kwa niaba ya wanafunzi washiriki wa Shindano hilo, Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) Yohana Lucas amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua nafasi kubwa ya vijana katika maendeleo ya Taifa na kuthamini dira ya Serikali katika kutengeneza kwa vijana kuchangia mawazo na ubunifu unaoweza kusaidia kutatua changamoto za jamii.
Katika shindano hilo, nafasi ya pili ilichukuliwa na kikundi cha wanafunzi watano kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), waliopata Shilingi milioni tano, huku Godson Jackson kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) akishika nafasi ya tatu na kujinyakulia Shilingi milioni tatu.
Mshindi wa nne alizawadiwa Shilingi milioni mbili, huku washindi wa tano hadi saba wakipata Shilingi milioni moja kila mmoja. Washindi wa nafasi ya nane hadi 10 walizawadiwa Shilingi laki tano kila mmoja. Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na kompyuta mpakato (laptop), vyeti na ngao.
Aidha, washindi wa nafasi ya 11 hadi 21 nao walipatiwa kompyuta mpakato pamoja na vyeti vya ushiriki.















No comments:
Post a Comment