TPDC na PURA hakikisheni Watanzania Wananufaika na Rasilimali za Mafuta na Gesi- MHE.SALOME - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 8, 2025

TPDC na PURA hakikisheni Watanzania Wananufaika na Rasilimali za Mafuta na Gesi- MHE.SALOME



Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amefanya ziara katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kuzungumza na Watendaji taasisi hizo mara baada ya kuteuliwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hiyo ambapo amewataka watendaji kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mhe. Salome ameweka mkazo kuhusu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania, huduma za kijamii na upatikanaji wa nishati kwa gharama nafuu.

Mhe. Salome pia ameielekeza Menejimenti ya TPDC kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi asilia majumbani ili Watanzania waendelee kunufaika zaidi na rasilimali hiyo muhimu.

Vilevile ameipongeza TPDC kwa jitihada wanazoendelea kufanya katika utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini kwani uboreshaji huo umeanza kuleta matokeo chanya katika upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali nchini huku akiwataka kuhakikisha jitihada hizo zinawanufaisha wananchi wengi zaidi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amewapongeza PURA kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuhakikisha sekta ya mafuta inakua nchini huku akiwahimiza kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki kwa wawekezaji wapya ili kuongeza ajira na kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na rasilimali na uwekezaji uliopo nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa miradi ya utafiti na uendelezaji wa gesi asilia, ikiwemo mradi wa LNG, ipewe kipaumbele ili kuongeza tija katika uwekezaji na kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali zake huku akisisitiza kuwa taasisi zote zilizo chini ya Wizara lazima ziweke mbele maslahi ya wananchi wakati wa kusimamia miradi ya kimkakati ya nishati lakini pia kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu usimamizi, matumizi na faida za rasilimali za gesi asilia.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amewasisitiza TPDC kuongeza kasi ya uzalishaji na upatikanaji wa gesi ili nishati hiyo iwe ya kutosha na inawafikia wananchi huku akiisisitiza PURA kuhakikisha wanawapa wawekezaji kipaumbele katika kuwekeza katika fursa za mafuta na gesi kwa lengo la kuhakikisha Serikali inapata mapato na wananchi wananufaika na miradi hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mussa Makame amesema shirika linaendelea kuimarisha miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha nishati ya mafuta na gesi, huku likiandaa vizuri upande wa maboresho ya masoko ili kuongeza ufanisi na upatikanaji wa bidhaa hizo nchini na kueleza kuwa kampuni ipo kwenye hatua za kufanya upanuzi wa miradi ya gesi, ikiwemo utekelezaji wa miradi midogo ya LNG itakayowezesha kusafirisha gesi hiyo katika mikoa mbalimbali kwa gharama nafuu na kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Eng. Charles Sangweni amesema PURA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku ikichangia kufanikisha malengo ya sekta kwa mujibu wa Dira ya Taifa 2050.





No comments:

Post a Comment