Benki Kuu ya Kenya (CBK) imewaonya wafanyabiashara wa maua na maduka ya zawadi dhidi ya kutengeneza shada la maua kwa kutumia noti.
Katika notisi ya umma ya Februari 2, 2026, CBK ilisema imeona ongezeko la matumizi ya noti kwa madhumuni ya mapambo, ikiwa ni pamoja na shada la pesa na maonyesho ya mapambo.
Video zimeenea kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaonyesha wamiliki wa maduka wakitengeneza mapambo kwa noti zilizokunjwa vizuri na kuungwa kulingana na rangi ya noti na thamani tofauti.
Benki Kuu inasema mtindo huo unaharibu sarafu ya Kenya na kuzifanya kuwa zisizofaa kwa mzunguko.
CBK ilisema hali hiyo pia inaathiri utendakazi mzuri wa vifaa vya kutunza na kuchakata fedha kama vile mashine za kutolea fedha (ATM), mashine za kuhesabu fedha na vifaa vya kuchambua pesa.
Benki Kuu iliongeza kuwa matokeo yake ni kukataliwa kwa pesa wakati wa kuchakata na kutoa pesa, kwa gharama inayoweza kuepukika kwa umma na benki.
Ingawa CBK ilisema haipingi kutoa pesa taslimu kama zawadi, ilihimiza kwamba zawadi hizo zisihusishe kubadilisha wala kuharibu noti kwa namna yoyote ile.
"Fedha inapaswa kusalia katika hali ambayo inaruhusu kuzunguka kwa uhuru na kutekeleza majukumu yake yaliyokusudiwa kama njia ya kubadilishana, na hifadhi ya thamani," CBK ilisema, na watengenezaji wanaweza kufungwa jela miaka saba iwapo watakamatwa.


No comments:
Post a Comment