
Na James K. Mwanamyoto - Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema jumla ya wanafunzi 937,581 waliopata alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300 wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104 ikijumuisha wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 3,228 wakiwemo wasichana 1,544 na wavulana 1,684 wamepangwa katika shule za sekondari za Serikali 5,230 kwa ajili ya kuanza masomo ya Kidato cha Kwanza mwaka, 2026.
Prof. Shemdoe hayo leo kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam, ambao ulilenga kutoa taarifa kwa umma kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi Januari, 2026.
Prof. Shemdoe ameanisha kuwa, shule walizopangiwa wanafunzi hao ni za bweni na za kutwa, ambapo shule za Sekondari za Bweni za Serikali zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni za wanafunzi wenye ufaulu wa Juu (Special Schools), za Amali na za bweni za kitaifa.
Prof. Shemdoa amesema, kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na Serikali, wanafunzi wote 937,581 wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104 waliofaulu Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi 2025 na kupangiwa shule wataanza muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka 2026 mnamo Januari 13, 2026.
Prof. Shemdoe amewaasa wanafunzi hao waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2026 nchini kuitumia vizuri fursa waliyoipata kwa kusoma kwa bidii ili wafikie malengo waliojiwekea na matarajio ya wazazi wao.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi na Watendaji wa Halmashauri kushirikiana na wadau wa elimu katika kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaanza masomo yao mwezi Januari, 2026 bila vikwazo vya aina yoyote ili kutekeleza azma ya Serikali ya utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo.
“Nawaagiza Ma RC, Ma RAS, Ma DC, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Shule kuhakikisha wanakamilisha maandalizi yote ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, ifikapo Januari 12, 2026 kwa wanafunzi waliochaguliwa shule za bweni na Januari 13, 2026 kwa wanafunzi waliochaguliwa shule za kutwa,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Aidha, Prof. Shemdoe amewahimiza wazazi, walezi na jamii kushirikiana na uongozi wa shule, mikoa, wilaya na halmashauri ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia shuleni hadi watakapohitimu elimu ya sekondari.
Orodha ya wanafunzi wote waliochaguliwa pamoja na Fomu za Maelezo ya Kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2026 (Joining Instructions) kwa Shule zote za Bweni zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI kupitia kiunganishi cha www.tamisemi.go.tz
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM -TAMISEMI) imekamilisha zoezi la Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kujiunga na Kidato cha Kwanza (K1) kwa mwaka wa masomo wa 2026 kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


No comments:
Post a Comment