Wajumbe wa Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Wizara ya Fedha, wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa ya ufuatiliaji na tathmini, ili iwe chombo cha kweli cha kuboresha maamuzi ya Wizara ya Fedha.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Huduma za Hazina na Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini Bw. Chotto Sendo, wakati akizindua Kamati hiyo ya wajumbe tisa (9) na kikao cha kwanza cha kamati, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Cate, mkoani Morogoro.
Bw. Sendo alisema kuanzishwa kwa Kamati hiyo ni hatua muhimu katika kutekeleza miongozo ya kitaifa ya usimamizi wa ufuatiliaji na tathmini inayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, na unaonesha dhamira ya Wizara katika kuimarisha utendaji unaozingatia matokeo.
‘‘Kwa Wizara ya Fedha, kuanzishwa kwa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini na sasa Kamati hii, ni uthibitisho wa dhamira ya Wizara kutafsiri miongozo ya kitaifa katika vitendo ambapo Kamati ina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Wizara, ikiwemo kufuatilia ufanisi wa taratibu, mifumo na zana za ufuatiliaji na tathmini, na kupendekeza maboresho stahiki,’’alisema Bw. Sendo.
Alisema Kamati hiyo ni chombo cha kitaalamu cha ushauri kwa Katibu Mkuu na Menejimenti ya Wizara inayopaswa kujadili taarifa za ufuatiliaji na tathmini kwa uwazi na uaminifu, kushauri hatua za maboresho, na kusimamia utekelezaji wa maamuzi yanayotokana na ushahidi pamoja na kusimamia utekelezaji wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Wizara.
Bw. Sendo alisisitiza kuwa Kamati hiyo si chombo cha utekelezaji wa moja kwa moja wa shughuli za Wizara, bali ni chombo cha kimkakati cha ushauri, usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maamuzi yanayotokana na taarifa za ufuatiliaji na tathmini.
‘‘Kamati hii itapimwa kwa mchango wake katika kuboresha ubora wa maamuzi ya Wizara, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, na uwajibikaji wa utendaji hivyo Wakuu wa Idara na Vitengo, ni muhimu kuhakikisha kuwa taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka maeneo yetu ni sahihi, kwa wakati, na zinatumika katika kupanga na kutekeleza shughuli’’, alisisitiza Bw. Sendo.
Bw. Chotto alisisitiza kuwa Kamati hiyo itakuwa chombo muhimu cha kuhakikisha kuwa agenda za kitaifa za ufuatiliaji na tathmini zinatekelezwa kikamilifu ndani ya Wizara ya Fedha, na kwamba masuala ya ufuatiliaji na tathmini yanatumika ipasavyo katika kufanya maamuzi, kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi na kuimarisha uwajibikaji kwa wadau wa wizara.
Aidha, Bw. Chotto alifafanua kuwa Kamati hiyo ni chombo cha kitaalamu cha ushauri kwa Katibu Mkuu na Menejimenti ya Wizara katika masuala ya ufuatiliaji na tathmini hivyo inawajibika kujadili taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Wizara, na kushauri hatua stahiki za kuchukua kwa kuzingatia ushahidi uliopo.
Aliongeza kuwa Kamati hiyo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo yanayotolewa na Katibu Mkuu au Afisa Masuuli kuhusiana na masuala ya ufuatiliaji na tathmini na kuhakikisha kuwa mapendekezo yanayotokana na taarifa za ufuatiliaji na tathmini yanatekelezwa kwa vitendo.
Bw. Sendo aliwapongeza Wakuu wa Idara na Vitengo kwa kuteuliwa na kukubali uteuzi huo wa kuwa wajumbe wa Kamati akieleza kuwa uteuzi huo unaakisi imani ya uongozi wa Wizara katika weledi, uzoefu na uwezo wao wa kuchangia kikamilifu kuimarisha utendaji unaozingatia ushahidi na matokeo.
Akizungumza kabla ya kumkaibisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini na Katibu wa Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini, Wizara ya Fedha, Bi. Theresia Henjewele, aliushukuru uongozi wa Wizara kwa kuanzishwa kwa Kamati hiyo ambayo itakuwa chombo muhimu cha kuimarisha matumizi ya ushahidi katika maamuzi ya Wizara.
Aidha, Bi. Henjewele alitoa wito kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Maafisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kushirikiana kwa karibu na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, kuhakikisha taarifa zinawasilishwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, ili ziweze kutumika kikamilifu katika ngazi ya Menejimenti.
Bi. Henjewele alisema kuwa Kwa mujibu wa muundo wa Wizara na miongozo ya kitaifa na ya Wizara, Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini ndicho chenye dhamana ya kitaasisi ya kusimamia na kuratibu masuala yote ya ufuatiliaji na tathmini ndani ya Wizara ya Fedha.
Alibainisha kuwa Kitengo kimeanza maandalizi ya ujenzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini, ambao unatarajiwa kuanza kutumika kikamilifu mwaka wa fedha 2026/27 sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa Kitengo na maafisa viungo wa ufuatiliaji na tathmini wa idara na vitengo ili kuongeza ufanisi, uwazi na matumizi ya taarifa kwa wakati.
Akizungumza kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati Elekezi ya Ufuatiliaji na Tathmini, Kamishna Msaidizi Idara ya Bajeti, Wizara ya Fedha, Bi. Vicky Jengo, alisema kuwa Kamati itafanya kazi yake kwa umahiri ikishirikiana na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini ili kuhakikisha kuwa ufuatiliaji na tathmini unaimarishwa katika Wizara na kuhakikisha Wizara inafikia malengo yake.









No comments:
Post a Comment