Na Augustina Makoye – WMJJWM Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa viongozi wa Majukwaa ya Wanaume nchini kuimarisha ushiriki wao katika kukuza usawa wa kijinsia na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano na Viongozi wa Jukwaa la Wanaume wa Mkoa wa Dodoma tarehe 23 Januari, 2023 jijini Dodoma, Waziri Gwajima amesema ushiriki wa wanaume ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Sera ya Taifa ya Jinsia ya mwaka 2023 na maendeleo jumuishi ya Taifa, ambayo imeweka mkazo kwenye ushirikishwaji wa wanaume katika masuala ya kijamii, uchumi, mazingira na utamaduni.
“Wanaume wana nafasi kubwa katika ustawi wa familia na jamii na endapo ushiriki wao utaendelea kuwa mdogo katika masuala ya kijinsia jitihada za Serikali na wadau katika kujenga jamii yenye usawa zitaendelea kudhoofika hivyo ni wakati wa wanaume kuwa sehemu ya suluhisho” amesema Dkt Gwajima.
Vilevile Waziri Gwajima amewahimiza viongozi wa majukwaa ya wanaume kuchukua nafasi yao kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na ubaguzi wa aina zote, akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia hauwezi kufikiwa bila ushiriki wa wanaume.
Waziri Gwajima amewapongeza viongozi wa majukwaa ya wanaume kwa jitihada zao na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha maendeleo jumuishi kwa wananchi wote kama yalivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amesema Wizara inaandaa mwongozo wa uratibu wa majukwaa ya wanaume ili kuleta tija zaidi ya mchango wao kwenye maendeleo na ustawi wa jamii kama ilivyobainishwa kwenye sera inayohusu masuala ya jinsia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanaume Mkoa wa Dodoma, Peter Mavunde amesema majukwaa hayo yamelenga kuwaunganisha wanaume, kujadiliana fursa na changamoto zinazowakabili, pamoja na kuandaa muongozo wa uratibu wa majukwaa hayo kuanzia ngazi ya Mkoa hadi vitongoji.
Ameongeza kuwa wamepokea maelekezo kutoka kwa Waziri na wataenda kuyafanyia kazi kwa vitendo, ikiwemo kuimarisha ushiriki wa wanaume katika masuala ya kijinsia, kupinga ukatili wa kijinsia na kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii.



No comments:
Post a Comment