
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kubakiza Riba ya Benki Kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026, ikilenga kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki ndani ya lengo.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati kilichofanyika tarehe 7 Januari 2026, kwa kuzingatia matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati iliyotolewa Januari 7,2026 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, uamuzi huo pia utawezesha ukuaji wa shughuli za kiuchumi kuwa wa kuridhisha.
Kutokana na uamuzi huo, Benki Kuu itaendelea kutekeleza sera ya fedha kwa kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.
UCHUMI WA DUNIA WAIMARIKA
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uchumi wa dunia uliendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha mwaka 2025 licha ya changamoto za ongezeko la ushuru wa forodha, migogoro ya kisiasa na kutokutabirika kwa hali ya uchumi wa dunia. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linakadiria uchumi wa dunia kukua kwa asilimia 3.2 mwaka 2025 na kuendelea kukua kwa kasi hiyo mwaka 2026.
Kamati imebainisha kuwa kushuka kwa bei ya mafuta ghafi hadi kufikia kati ya dola za Marekani 62 hadi 65 kwa pipa, kunatarajiwa kuendelea kupunguza mfumuko wa bei na mahitaji ya fedha za kigeni nchini. Aidha, ongezeko la bei ya dhahabu duniani linatarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuimarisha zaidi thamani ya shilingi ya Tanzania.
UCHUMI WA NDANI WAENDELEA KUKUA
Kwa upande wa uchumi wa ndani, Kamati ilieleza kuwa uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa takriban asilimia 5.9 mwaka 2025, ukichangiwa zaidi na sekta za kilimo, madini na ujenzi. Zanzibar inatarajiwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2026, huku sekta za ujenzi, utalii na viwanda zikiwa vinara wa ukuaji huo.
Mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu, ambapo katika robo ya nne ya mwaka 2025 ulikuwa asilimia 3.5 Tanzania Bara na asilimia 3.4 Zanzibar. Kamati inatarajia hali hiyo kuendelea katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.
Sekta ya benki imeendelea kuwa imara, ikiwa na ukwasi na mtaji wa kutosha, huku uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ukipungua hadi asilimia 3.1, chini ya kiwango cha juu kinachovumilika cha asilimia 5.
SEKTA YA NJE NA FEDHA ZA KIGENI
Sekta ya nje imeendelea kuimarika, ambapo nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inakadiriwa kupungua hadi asilimia 2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2025, kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka mitano. Akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.3, kiasi kinachoweza kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kwa takribani miezi 4.9.
Kwa upande wa sera ya bajeti, makusanyo ya kodi yameendelea kuongezeka na deni la Serikali limeendelea kuwa himilivu, likiwa chini ya ukomo unaokubalika kimataifa.
Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kukutana tena tarehe 2 Aprili 2026, ambapo tangazo la Riba ya Benki Kuu kwa robo ya pili ya mwaka 2026 litatolewa tarehe 3 Aprili 2026.

No comments:
Post a Comment