Na Sixmund Begashe, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amezitaka sekta binafsi, asasi za kiraia, wawekezaji na jamii zinazozunguka hifadhi kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza sekta za Misitu, Ufugaji Nyuki na Malikale, kwa kuwa sekta hizo ni chanzo cha ajira rasmi na ni nguzo muhimu za uchumi wa nchi, jamii, na uhifadhi endelevu wa Mazingira.
Dkt. Kijaji ameyabainisha hayo, jijini Dodoma, kwenye kikao chake na Wadau wa sekta hizo chenye lengo la kupata uelewa wa pamoja wa maendeleo yake endelevu.
Ameeleza kuwa chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Sekta ya Misitu inachangia takriban asilimia 3.5 ya pato ghafi la Taifa
"Kutokana na umuhimu wake, Wizara imefanikiwa kuandaa jumla ya mipango 235 ya kusimamia hifadhi za misitu, mipango 24 ya usimamizi wa mashamba ya miti na mipango 259 ya mashamba ya ufugaji nyuki". Alisema Dkt. Kijaji.
Amesema kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa misitu imeendelea kuimarisha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta ya hiyo hatua iliyopelekea kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji wa malighafi mbao katika mashamba ya Serikali yanayolimwa miti kibiashara kutoka mita za ujazo 1,108,791 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia mita za ujazo 1,264,535 mwaka 2024/2025.
Kwa upande wa Ufugaji Nyuki Dkt. Kijaji amebainisha kuwa taifa linaendelea kushuhudia ongezeko la mauzo ya asali nje ya nchi kutoka tani 607 zenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 Mwaka 2021 hadi kufikia tani 1,713 zenye thamani ya shilingi bilioni 18.6 mwaka 2025
Katika kuleta mageuzi makubwa ya Sekta ya Malikale, Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imewezesha kutambua na kutangaza maeneo ya malikale 25 ambayo yatatumika kama vivutio vya utalii nchini.
"Katika mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya maeneo 15 yametambuliwa na kukidhi vigezo vya kuwa Urithi wa Taifa ambapo taratibu za kuyatangaza zinaendelea". Alieleza Dkt. Kijaji
Aidha licha ya kuwapongeza wadau hao, Dkt. Kijaji amewahakikishia kuwa, Wizara yake itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega kwa maslahi mapana ya sekta hizo na Taifa kwa ujumla.
Kikao hicho, kimeudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii Bw. Nkoba Mabula, Viongozi wa Idara, Vitengo na taasisi za Wizara hiyo.




No comments:
Post a Comment