Na OWM - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro kutupa takataka katika barabara za Muhimbili, Tubuyu II, Mjimwema, Barakuda na Kihonda-VETA zenye urefu wa Kilomita 12.85 ambazo zimejengwa na Serikali kupitia na Mradi wa TACTIC ikizingatiwa kuwa barabara hizo bado hazijakabidhiwa rasmi.
Prof. Shemdoe amekemea kitendo hicho cha baadhi ya wananchi kutothamini miundombinu hiyo ya barabara, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa TACTIC katika Manispaa ya Morogoro.
“Zimejengwa barabara nzuri sana lakini wananchi wenzangu mmeanza kutumia barabara hizi kama dampo la kutupa takataka, na si jambo jema kuendelea kutupa takataka wakati hatujakabidhiwa barabara,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amemtaka Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Khalid Matengo kutoa elimu kwa wananchi ya kuacha kutupa takataka katika miundombinu hiyo ya barabara badala yake kuilinda, kuitunza ili itumike kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya taifa.
Ameongeza kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha ujenzi wa barabara hizo ili ziinufaishe jamii, hivyo wananchi wanapaswa kumheshimisha Mheshimiwa Rais kwa kuzitunza barabara zote zilizojengwa ili zitumike kwa muda mrefu.
“Mstahiki Meya atakayekamatwa ametupa takataka ngumu kwenye mitaro ya barabara atozwe faini kwa mujibu wa sheria na taratibu za Manispaa mlizojiwekea, naomba suala hili ulifuatilie kwa ukaribu Mhe. Mstahiki Meya,” Prof. Shemdoe amehimiza.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetumia fedha nyingi kiasi cha Shilingi Bilioni 19.6 kujenga barabara hizo zenye urefu wa kilomita 12.85 hivyo zinapaswa kulindwa ili ziendelee kuleta tabasamu kwa wananchi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa TACTIC, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Mboka Nkwera amesema mradi huo mmoja wa TACTIC utekelezaji wake umefikia asilimia 94.51 na kwa sasa mkandarasi anaendelea kukamilisha kazi ndogondogo za umaliziaji wa mifereji, kuweka vivuko pamoja na taa za barabarani.
Kwa upande wake, mkazi wa Manispaa ya Morogoro Bw. Jafari Kilala ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga miundombinu imara ya barabara katika Manispaa hiyo na kuongeza kuwa wananchi wameridhishwa na kiwango cha barabara zinazojengwa.
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa miji 45 ambayo imenufaika na ufadhili wa mradi huo wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji, Manispaa na Majiji (TACTIC) unaotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kupitia TARURA.







No comments:
Post a Comment