Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew ameiagiza kampuni ya Megha Engineering and Infrastructure LTD kuwasilisha mpango kazi unaoonesha namna mradi wa maji wa miji 28 Kasulu utakavyokamilika ifikapo Julai mwaka huu.
Amesema mpango kazi huo unatakiwa kulenga kutumia miezi miwili pekee kutandaza mabomba yenye urefu wa kilometa 42 katika maeneo mbalimbali ya huduma ili kuharakisha upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi huo wilayani Kasulu, ambapo alieleza kuwa awali mradi huo ulipaswa kukamilika Oktoba mwaka jana kabla ya mkandarasi kuomba kuongezewa muda hadi Julai mwaka huu.
Naibu Waziri amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona mradi unakamilika kwa wakati ili kuwaondolea wananchi wa Kasulu adha ya kubeba ndoo kichwani, hivyo Wizara ya Maji haina nia ya kuendelea kusogeza mbele muda wa utekelezaji.
Aidha, amewapongeza wakandarasi kwa kufanya manunuzi ya vifaa muhimu vya utekelezaji ambavyo amevishuhudia katika eneo la mradi, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika hatua nyingine muhimu za kazi.
Mradi wa maji wa miji 28 Kasulu unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 35, umefikia asilimia 57 ya utekelezaji na unatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 187,000 mara utakapokamilika.






No comments:
Post a Comment