Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewasilisha Ripoti ya Utafiti wa Ufanisi wa Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), katika Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma, Januari 22, 2026.
Ripoti hiyo, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Profesa Leonarda Mwagike, imeonesha kuwa utekelezaji wa Mfumo wa NeST umeleta mafanikio makubwa katika kuongeza uzingatiaji wa sheria na taratibu za ununuzi wa umma, kupanua wigo wa upatikanaji wa thamani halisi ya fedha, kuhakikisha uwazi na haki kwa wazabuni wa Kitanzania, pamoja na kuimarisha usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma nchini.
Akizungumza mbele ya Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, alisema kuwa Mfumo wa NeST umechangia kwa kiasi kikubwa kuokoa fedha zilizokuwa zinatumika katika uchapishaji wa nyaraka za zabuni. Aidha, alieleza kuwa mfumo huo umepunguza athari za kimazingira kwa kuondoa uchomaji wa karatasi na kupunguza safari zisizo za lazima za wazabuni waliokuwa wakisafiri kwenda kuwasilisha nyaraka kwa njia ya kawaida.
Bw. Simba aliongeza kuwa tangu kuanza kutumika kwa Mfumo wa NeST, makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu yamefanikiwa kupata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 32, hatua inayodhihirisha mchango wa mfumo huo katika kukuza ushirikishwaji, usawa na ujumuishi katika ununuzi wa umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Mheshimiwa Ado Shaibu, kwa niaba ya Kamati, aliipongeza PPRA kwa ujenzi na usimamizi madhubuti wa Mfumo wa NeST. Alisisitiza umuhimu wa PPRA kuendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wadau wote wa ununuzi wa umma kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na matumizi sahihi ya Mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika sekta hiyo.






No comments:
Post a Comment