RAIS SAMIA AMEIMARISHA UCHUMI GEITA KUPITIA UJENZI WA BARABARA YA KASAMWA-GAMASHI - PROF. SHEMDOE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, January 25, 2026

RAIS SAMIA AMEIMARISHA UCHUMI GEITA KUPITIA UJENZI WA BARABARA YA KASAMWA-GAMASHI - PROF. SHEMDOE


Na OWM - TAMISEMI, Geita


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Shilingi 1,035,047,200/= za ujenzi wa dharura wa barabara ya Kasamwa- Gamashi yenye urefu wa kilomita 18, iliyoimarisha shughuli za kiuchumi kupitia Sekta ya Usafiri na Usafirishaji kati ya Wilaya ya Nyang’hwale na Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.

Prof. Shemdoe amesema barabara hiyo ina umuhimu kiuchumi kwa wananchi wa Nyang’hwale na Geita ambao wanategemea shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo uzalishaji unaofanyika Nyang’hwale ulikuwa hauwezi kufika makao makuu ya mkoa kutokana na changamoto iliyokuwepo ya ubovu wa miundombinu ya barabara ya  Kasamwa- Gamashi.

“Ujenzi wa barabara hii ni muhimu sana kiuchumi, hivyo tunapaswa kumshukuru Mhe. Rais kwa kuidhinisha fedha zilizowezesha barabara kujengwa ili kuendeleza shughuli za wananchi kiuchumi,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amempongeza Mshauri Elekezi kampuni ya Norplan Tanzania Ltd kwa usimamizi mzuri wa mradi huo  akiwa ni mwakilishi wa mshitiri, na kuongeza kuwa Washauri Elekezi wote wangetekeleza wajibu wao kama alivyotekeleza Norplan Tanzania Limited, kusingekuwa na malalamiko wala changamoto ya miradi kusuasua.

Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza Mkandarasi wa mradi huo kampuni ya Madata Investment Ltd kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo uliofikia asilimia 82 kwa kutumia fedha yake mwenyewe, na kuanisha kwamba wakandarasi wa aina ya Madata Investment wakipatikana kutakuwa hakuna miradi mingi inayosuasua.  

“Nakupongeza sana mkandarasi kwa kazi nzuri uliyoifanya katika mradi huu, na ninakuhakikishia kuwa fedha ya kukulipa ipo, wewe lete maombi ulipwe lakini nakuomba uzingatie Februari 27, 2026 unapaswa kukabidhi mradi huu,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita, Mhandisi Bahati Subeya amesema mradi huo wa ujenzi wa dharura katika barabara ya Kasamwa- Gamashi ulianza rasmi Agosti 25, 2025 na unatarajiwa kukamilika Februari 27, 2026.

Mhandisi Subeya amefafanua kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaboresha sekta ya usafiri na usafirishaji pamoja na shughuli za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo za afya na elimu.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Grace Kingalame amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa barabara ya Kasamwa- Gamashi ambayo itaondoa changamoto ya mawasiliano kati ya wilaya yake na makao makuu ya mkoa, na kuongeza kuwa wananchi wa Nyang’wale na Geita wanafurahishwa na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kuwaletea maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Mradi huo wa Barabara ya Kasamwa- Gamashi, ni miongoni mwa miradi tisa (9) yenye thamani ya Shilingi 4,015,469,549/= inayotekelezwa na TARURA mkoa wa Geita kupitia Mradi wa CERC (Contingency Emergency Response Component) - DMDP II unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambao unatokana na barabara  zilizoathiriwa na mvua za Elnino mwaka 2023.

No comments:

Post a Comment