Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amewapongeza makandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa barabara na madaraja katika mikoa ya Geita na Shinyanga kwa kuzingatia kasi na ubora.
Amesema Serikali imedhamiria kuwawezesha makandarasi na wasimamizi wa miradi ya ujenzi wazawa ili kuwajenge uwezo,ujuzi,uzoefu na kukuza ajira nchini.
" Ni fahari kwa taifa miradi hii ya dharura kujengwa na wazawa na kukamilika kwa wakati na ubora hatua inayoongeza imani ya Serikali kwa makandarasi wazawa", amesisitiza Eng. Kasekenya.
Amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza wigo kwa makandarasi wazawa wenye uwezo kutoka shilingi bilioni 10 hadi 50 hivyo wale watakaokabidhi kazi nzuri na bora wataaminiwa kupewa miradi mikubwa.
Akiwa mkoani Geita Eng. Amekagua ujenzi wa barabara kuu ya Wendele-Mlele na Barabara ya mkoa kutoka Kashelo-Masumbwe-Mwabomba ambazo baada ya kuathiria na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya sasa zimejengwa upya.
Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Geita Eng. Vedastus Maribe amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa ujenzi madaraja na barabara chini ya mpango wa dharura utakamilika Januari 31.
Mkoani Shinyanga Eng. Kasekenya amekagua barabara inayou unganisha mkoa wa Geita-Shinyanga -Tabora kupitia Ushetu ambapo madaraja ya Kasenga 80mita, Ubagwe 60 mita na Ng'hwande yalioharibiwa na El-nino yamekamilika.
Meneja wa TANROADS Shinyanga Eng. Ntuli Mwaikokesya amesema wanajipanga kufunga taa kwenye madaraja hayo ili kuimarisha usalama na kupendezesha eneo la Ushetu.
Wakandarasi wazawa waliopongezwa ni pamoja na Samota, Jonta Investment, M/s Jossam na M/s Mumangi ambao wote wamesimamiwa na TECU - Geita na Shinyanga.
Naibu Waziri Kasekenya anaendelea na ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa kukagua ujenzi wa barabara na madaraja yanayojengwa chini ya mpango wa dharura.









No comments:
Post a Comment