
Afisa Mkuu Uendelezaji wa Fedha Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bw. Fred Ilomo, akitoa elimu ya fedha kwa kikundi cha Wanawake na Samia kuhusu usimamizi wa fedha binafsi yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi".

Mkazi wa Jiji la Tanga, Bi. Mariam Kazandi akielezea namna alivyoelewa kuhusu madhara ya mikopo kausha damu wakati akipatiwa elimu ya fedha na wataalam kutoka Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

Baadhi ya wanakikundi cha Wanawake na Samia jijini Tanga, wakipatiwa elimu kuhusu usimamizi wa fedha binafsi na wataalam kutoka Wizara ya Fedha ikiwa ni maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.

Mkazi wa Jiji la Tanga, Bi. Shamsa Mputila akielezea namna alivyoelewa kuhusu madhara ya mikopo “kausha damu” wakati akipatiwa elimu ya fedha na wataalam kutoka Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya tano, yenye kaulimbiu "Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi" yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, Jijini Tanga.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Tanga)
Na. Chedaiwe Msuya na Eva Ngowi, WF, Tanga
Katika mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Usagara jijini Tanga, leo 24 Januari, 2026, kikundi cha Wanawake na Samia kutoka jiji hilo kimejitokeza kushiriki na kupata elimu ya fedha inayotolewa na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha.
Maadhimisho haya yanalenga kutoa uelewa mpana kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za kifedha, ikiwa ni pamoja na kuweka akiba, kukopa kwa uangalifu na kupanga matumizi ya fedha kwa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Mkuu Uendelezaji wa Fedha Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Bw. Fred Ilomo, aliwataka wanawake hao kutumia fursa hiyo kujifunza na kujiimarisha kiuchumi kupitia maarifa wanayoyapata, akisisitiza kuwa elimu ya fedha ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya familia na taifa.
Wanawake hao walipatiwa mafunzo kuhusu namna ya kuendesha miradi midogo na ya kati, matumizi ya huduma za benki na taasisi za fedha, pamoja na umuhimu wa kuwa na mipango ya kifedha iliyo bora.
Akiongea kwa niaba ya wanawake wa kikundi cha Wanawake na Samia Bi. Stella Luther Malingwi alisema, wamefurahishwa na mafunzo waliyopewa, wakisema yamewasaidia kuelewa kwa vitendo jinsi ya kusimamia mapato yao, kuepuka mikopo isiyo na tija na kutumia fursa za kifedha zilizopo kwa maendeleo yao.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma ya Fedha yanatarajiwa kuendelea katika viwanja hivyo hadi tarehe 26 Januari, 2026, yakihusisha makundi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kujenga jamii yenye uelewa mpana wa masuala ya kifedha.

No comments:
Post a Comment