SERIKALI YACHUKUA HATUA KUTATUA CHANGAMOTO ZA UFADHILI WA MASOMO NJE YA NCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 20, 2026

SERIKALI YACHUKUA HATUA KUTATUA CHANGAMOTO ZA UFADHILI WA MASOMO NJE YA NCHI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika Januari 20, 2025, Jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyika Januari 20, 2025, Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, akizungumza wakati wa kikao kazi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilichofanyik


Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG - DODOMA


Serikali imeanza kuchukua hatua mahsusi za kutatua changamoto ya upatikanaji wa ufadhili wa masomo nje ya nchi baada ya kubaini kuwa wanafunzi wengi wa Kitanzania wanakosa fursa hizo kutokana na kushindwa kuziomba ipasavyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Januari 20, 2026 jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi kati ya Wizara hiyo na taasisi zilizo chini yake.

Prof. Mkenda amesema Serikali imefanikiwa kupata nafasi 127 za ufadhili wa masomo nchini Saudi Arabia, lakini bado idadi ya wanafunzi wanaoomba na kunufaika na fursa hizo ni ndogo, hali iliyosababisha Wizara kuanza kushughulikia vikwazo vinavyowafanya wanafunzi wengi kushindwa kuomba masomo nje ya nchi.

Amesema Wizara imeanza mchakato wa haraka wa kufanya tathmini ili kubaini sababu zinazofanya Watanzania kutozitumia kikamilifu fursa za masomo nje ya nchi pindi zinapojitokeza, akisisitiza kuwa hali hiyo haikubaliki ikizingatiwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata elimu katika vyuo vya nje ya nchi.

“Ni muhimu kubaini kwa nini fursa zinapopatikana hazichangamkiwi na Watanzania, ili Serikali iweze kuchukua hatua sahihi na kuongeza ushiriki wa wanafunzi wetu katika masomo ya kimataifa,” amesema Prof. Mkenda.

‎Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema kuwa kikao hicho ni fursa muhimu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa sera na mipango ya Wizara.

‎Aidha amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa Wizara, taasisi zake na wataalamu wa sekta ya elimu ili kuhakikisha mageuzi yanayopangwa yanatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.

Naye , Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kikao kazi hicho kinalenga pia kujadili kwa kina namna watumishi wa Wizara na taasisi zilizo chini yake watakavyotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika sekta ya elimu.

Prof. Nombo amebainisha kuwa utekelezaji wa dira hiyo unahitaji mshikamano, ubunifu na mipango thabiti itakayowezesha elimu ya Tanzania kuendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye, ikiwemo kuongeza idadi ya wataalamu waliopata elimu na uzoefu wa kimataifa.

Kikao hicho kinatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa kisera na kiutendaji katika kukuza fursa za masomo nje ya nchi na kuboresha mchango wa sekta ya elimu katika maendeleo ya Taifa.





No comments:

Post a Comment