SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 10.5 KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, January 25, 2026

SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 10.5 KUWAWEZESHA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO




Na Okuly Julius, OKULY BLOG - Dodoma


Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo nchini, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya Siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika awamu ya sita, kipindi cha pili cha uongozi wake.

Akizungumza leo Januari 25, 2026, jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kati ya fedha hizo, jumla ya Shilingi bilioni 1.35 tayari zimetolewa kwa wafanyabiashara ndogondogo 588 kupitia Benki ya NMB, huku zoezi la utoaji mikopo likiendelea nchi nzima. Mikopo hiyo inatolewa kwa riba nafuu ya asilimia saba (7) kwa mwaka.

Aidha, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Serikali imetoa Shilingi milioni 337.97 kwa wanawake wajasiriamali 45 kwa riba ya asilimia nne (4), hatua inayolenga kuongeza uwezo wa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Wafanyabiashara 119,595 Warasimishwa
Dkt. Gwajima amesema katika kipindi cha siku 100, Wizara imesajili jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 119,595 katika Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBNMIS), ambapo wanawake ni 73,341 na wanaume 46,254.

Ameeleza kuwa kati ya waliosajiliwa, Machinga ni 103,102, Mama na Baba Lishe 12,384, pamoja na waendesha bodaboda na bajaj 4,109, hatua iliyowawezesha kuingia kwenye mifumo rasmi na kunufaika na fursa za kiuchumi.

Kwa upande wa urasimishaji wa waendesha vyombo vya moto, Waziri amesema kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jumla ya waendesha pikipiki na bajaj 209,632 wamerasimishwa kwa kupatiwa leseni za udereva, huku akihimiza wengine kujitokeza ili wanufaike na huduma na fursa zinazotolewa na Serikali.

Ameongeza kuwa kupitia Wezesha Portal chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, vikundi 6,041 vya wajasiriamali vimesajiliwa, vikiwemo vikundi vya wanawake 3,207, vijana 2,318 na watu wenye ulemavu 516, vyenye jumla ya wanufaika 30,205.

Usajili huo umewezesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri yenye thamani ya Shilingi bilioni 33.45 kwa vikundi 3,776, ambapo vikundi vya wanawake vimepata Shilingi bilioni 15.68, vijana Shilingi bilioni 16.23, na watu wenye ulemavu Shilingi bilioni 1.53.

Dkt. Gwajima amesema kupitia ushirikiano na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na SIDO, wajasiriamali 16,325 wamerasimishwa, 11,000 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na 12,325 wakipata mikopo ya kukuza mitaji, huku zaidi ya 3,900 wakipatiwa TIN na leseni za biashara.

Ameeleza kuwa benki mbalimbali zimeendelea kushirikiana na Serikali, ambapo kupitia Benki ya NMB, wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali 511,898 wamenufaika na mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 646.76, Benki ya TCB ikitoa Shilingi bilioni 56.1, na DCB kutoa Shilingi bilioni 4.53.

Kuhusu masoko, Waziri amesema Serikali kupitia PPRA imerasimisha vikundi 1,216 vya makundi maalum katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST), hali iliyowezesha vikundi 1,123 kupata zabuni za manunuzi ya umma zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kutenga asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi maalum.

Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga uchumi jumuishi, unaowajali wafanyabiashara ndogondogo, wanawake, vijana na makundi maalum.

No comments:

Post a Comment