KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA KIWANDA CHA NGUZO ZA ZEGE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 12, 2026

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA KIWANDA CHA NGUZO ZA ZEGE


Na Mwandishi wetu, Tabora


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na Ujenzi wa Kiwanda cha Zege kinachomilikiwa na kampuni tanzu ya TANESCO ya kuzalisha nguzo za zege kilichopo katika Mkoa wa Tabora wakati wa ziara yao ya kikazi Mkoani humo tarehe 12 Machi, 2026.


Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Subira Mgallu ameeleza kuridhishwa na hatua ya kukamilika kwa Kiwanda hicho kilichoanza uzalishaji na kuwaelekeza Wizara ya Nishati na TANESCO kukisimamia kiwanda hiko kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuzalisha faida.

"Kwa niaba ya Kamati tumeridhika na kazi kubwa iliyofanyika katika kiwanda hiki ambacho kimekamilika na uzalishaji umeanza, tunatoa rai kwa Wizara na TANESCO kuendelea kusimamia kiwanda hiki ili kiendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi", alieleza Mhe. Mgallu

Alieleza kuwa uelekeo wa sasa ni kusambaza nguzo za zege hasa kwa maeneo yenye unyevu sambamba na maeneo yaliyo karibu na misitu pamoja na mikondo ya mito ya maji ambayo nguzo za miti huathirika kwa kiasi kikubwa haswa kwenye msimu wa mvua hivyo nguzo za zege zitakuwa msaada mkubwa katika mazingira kama hayo na kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme.

“Kama mnavyofayahamu kwa sasa uelekeo ni kusambaza nguzo za zege badala ya nguzo za miti hasa katika maeneo ambayo yana asili ya unyevu, maeneo karibu na mito ya maji ama visiwa ambapo nguzo za miti huathiriwa na mazingira hayo”, aliongeza.


Naye Mhe. Deogratius Ndejembi Waziri wa Nishati alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hiko umekamilika mwaka huu na kuanza uzalishaji wake rasmi Februari, 2026 ambapo mpaka sasa wastani wa nguzo zinazozalishwa ni 80 hadi 120 kwa siku ambapo mpaka sasa gharama ya shilingi bilioni 6.4 imeshatumika katika hatua zote hadi uzalishaji ulipoanza ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.4 bado hazijalipwa kwa mkandarasi ambaye bado yupo kwenye kipindi cha uangalizi.

“Kiwanda hiki kilianza uzalishaji rasmi mwezi Februari mwaka huu ambapo kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha nguzo 80 hadi 120, mpaka sasa ujenzi wa kiwanda hiki hadi uzalishaji ulipoanza imetumia gharama ya shilingi bilioni 6.4 ambapo bado kuna billioni 1.6 bado haijalipwa kwa mkandarasi kwa kuwa yupo kwenye kipindi cha uangalizi”, aliongeza Mhe. Ndejembi. 


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange ameeleza kuwa kukamilika kwa kiwanda hiko kunaenda kuleta mageuzi makubwa kwani nguzo za zege ni teknolojia ambayo bado inakuwa hivyo Shirika bado linaendelea kuikuza sekta na kuwa na utoshelevu wa nguzo zenyewe kwa matumizi ya wananchi. 

“Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda na kuanza uzalishaji ambapo kwa hali ilivyo ya matumizi ya nguzo za zege ni teknolojia ambayo bado inakuwa hivyo kama Shirika tutahakikisha tunaisimamia sekta hii ili kuendelea kuwapatia wateja wetu huduma ya umeme wa uhakika”, alisema Bw. Twange.

Ziara hiyo ya kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini inalenga kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Shirika katika maeneo mbalimbali nchini ili kujionea ufanisi wake.

No comments:

Post a Comment