SIKU 100 ZA RAIS SAMIA: KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA KASI YA WIZARA YA NISHATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, January 20, 2026

SIKU 100 ZA RAIS SAMIA: KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA KASI YA WIZARA YA NISHATI


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
Mhe.Subira Mgalu akizungumza wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha
taarifa kuhusu Sera, Sheria, Muundo na Majukumu ya Wizara ya Nishati
katika kikao cha kwanza kati ya Kamati hiyo na viongozi wa Wizara ya
Nishati pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya
Nishati kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya siku 100 za
uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuanza kusambaza
umeme katika vitongoji 9,009, hatua inayoonesha mwelekeo chanya wa
utendaji wa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 20, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, wakati wa kikao cha kwanza kati ya
Wizara ya Nishati, taasisi zilizo chini yake pamoja na Kamati hiyo.

Kikao hicho kimelenga kuijengea Kamati uelewa kuhusu muundo na
majukumu ya Wizara ya Nishati, pamoja na sera na sheria mbalimbali
zinazosimamiwa na Wizara hiyo katika kuendeleza Sekta ya Nishati
nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mgalu amesema mafanikio
yaliyopatikana ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia ni ushahidi
wa dhamira ya Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya
uhakika kwa wananchi.

“Niwapongeze sana Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa kazi nzuri
mnayoendelea kuifanya katika kuijenga Sekta ya Nishati. Mafanikio haya
yamejidhihirisha wazi ndani ya siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan. Tumeshuhudia uzinduzi wa Kituo cha Umeme cha
Mtera ambacho kitaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Dodoma
na Iringa, pamoja na uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika
vitongoji 9,009 nchini,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema
Wizara itaendelea kuhakikisha Sekta ya Nishati inachangia ipasavyo
katika kufikiwa kwa malengo ya kitaifa na kimataifa, sambamba na
kukuza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa
wananchi.

Amebainisha Serikali itaendeleza matumizi ya vyanzo mbalimbali vya
nishati ambavyo Tanzania imebarikiwa navyo ili kufanikisha mpango wa
kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030, pamoja na
kuongeza matumizi ya umeme kwa wananchi hadi kufikia wastani wa
kilowati saa (KWh) 3,000 kwa kila mtu ifikapo mwaka 2050.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhe. Ndejembi amesema Wizara
inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya
nishati safi ya kupikia, kuongeza vituo vya upatikanaji wa nishati
hiyo pamoja na kubuni na kuendeleza teknolojia rafiki kwa mazingira.

Aidha, ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na
Kamati hiyo na kuzingatia maoni na ushauri wa Kamati hiyo katika
utekelezaji wa majukumu yake kwa maendeleo ya Sekta ya Nishati na
Taifa kwa ujumla.

Viongozi wengine wa Wizara ya Nishati waliohudhuria kikao hicho ni
pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, pamoja na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

No comments:

Post a Comment