UZINDUZI WA KITUO CHA KUP0ZA NA KUSAMBAZA UMEME CHA MTERA KUIMARISHA HUDUMA KATIKA KANDA YA KATI NA KUSINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, January 15, 2026

UZINDUZI WA KITUO CHA KUP0ZA NA KUSAMBAZA UMEME CHA MTERA KUIMARISHA HUDUMA KATIKA KANDA YA KATI NA KUSINI


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy, amesema kuwa uzinduzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Mtera ni hatua muhimu na ya kimkakati katika kuboresha upatikanaji na uhakika wa umeme katika wilaya za Kongwa, Mpwapwa pamoja na mikoa ya Dodoma na Iringa kwa ujumla.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 15, 2026, katika Makao Makuu ya REA jijini Dodoma, Mha. Saidy amesema uzinduzi rasmi wa kituo hicho utafanyika Januari 16, 2026 jijini Dodoma na utaongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deo Ndejembi. 


Ameeleza kuwa tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati Vijijini unaolenga kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wote bila kujali wanakoishi.


Mha. Saidy amesema kuwa kituo hicho kimejengwa kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 9.7, fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali za Sweden na Norway.


 Amebainisha kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumewezesha kupunguza tatizo la umeme hafifu (low voltage), kupunguza kukatika kwa umeme kwa kiasi kikubwa, na kuimarisha usambazaji wa umeme kutoka Mtera hadi Dodoma na Iringa.


Ameongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho umehusisha transfoma mbili za kiwango cha MV kumi kila moja, chumba cha “Swaggz Room” kwa ajili ya njia za umeme, pamoja na mifumo ya “Break Control” na “Communication System.” Kwa mujibu wa Mha. Saidy, miundombinu hiyo itaongeza uwezo wa TANESCO katika kusambaza umeme kwa ufanisi zaidi na kutoa huduma bora kwa wananchi, viwanda vikubwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.



Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa REA inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji zaidi ya 9,000 kote nchini. 

Ameeleza kuwa tangu mwaka 2021 hadi sasa, vitongoji 28,000 tayari vimeunganishwa na umeme, huku vitongoji 13,445 vikiwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya takribani shilingi trilioni 1.2 na unatarajiwa kutoa ajira zisizopungua 4,600 moja kwa moja kwa wananchi wa vijijini.


Mha. Saidy pia amebainisha kuwa REA ina mpango wa kujenga vituo vidogo vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mtwara, Hanang, Nzega na Mbarali, ambapo taratibu za awali zikiwemo za kujenga vyuo katika maeneo hayo zinaendelea. 


Amefafanua kuwa lengo la REA ni kuhakikisha kila wilaya nchini Tanzania inakuwa na kituo kidogo cha kupoza umeme ili kuboresha zaidi upatikanaji na uhakika wa huduma hiyo.


Ameongeza kuwa miradi hiyo itawezesha kuunganishwa kwa miundombinu muhimu ya kijamii ikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na pampu za maji, hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijijini. 


Amehimiza wananchi kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme kuboresha maisha yao na kukuza shughuli za uzalishaji.


Kwa upande mwingine, Mha. Saidy amesema kuwa REA inatarajia kusaini mikataba ya utekelezaji wa mradi mwingine mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji takribani 9,000 kote nchini. Tukio hilo linatarajiwa kufanyika Jumamosi Januari 17, 2026 katika Ukumbi wa Hazina Ndogo jijini Dodoma. 


Amesema mradi huo utatekelezwa kupitia mafungu 30 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu.


Akihitimisha, Mha. Saidy amesema kuwa mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia Watanzania wote na kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.






No comments:

Post a Comment