WAKULIMA DODOMA: UTEKELEZAJI WA AHADI ZA COP30 KILIMO KIPEWE KIPAOMBELE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, January 25, 2026

WAKULIMA DODOMA: UTEKELEZAJI WA AHADI ZA COP30 KILIMO KIPEWE KIPAOMBELE


Na Asha Kamata, Dodoma


Hali ya ukame na mvua zisizotabirika imeendelea kuwa changamoto sugu katika maeneo mengi nchini hali inayosababisha wakulima kupata hasara kubwa kutokana na misimu ya kilimo isiyo na uhakika. Wakulima wengi huvuna mazao machache huku wengine wakikosa kabisa, jambo linalotishia usalama wa chakula na kipato cha kaya.

Kutokana na hali hiyo, wakulima wa mkoa wa Dodoma wameiomba serikali kuharakisha utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliohitimishwa Novemba 22, 2025 nchini Brazil, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya uvunaji wa maji ya mvua na kuanzishwa kwa bima ya kilimo.

Katika mkutano huo, Tanzania ilitajwa miongoni mwa nchi zilizopata ahadi ya ufadhili wa takribani dola milioni 20 (sawa na shilingi bilioni 48) kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambapo sekta ya kilimo ilipewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa wakulima, fedha hizo zinapaswa kuelekezwa kwenye miradi ya uvunaji wa maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, pamoja na kuanzishwa kwa bima itakayowalinda dhidi ya hasara zinazotokana na ukame na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkulima kutoka wilaya ya Bahi, Samwel Mlugu na Agustino Ndonuu, wanasema uvunaji wa maji ya mvua utaongeza ustahimilivu wa kilimo katika maeneo yao ambayo hutegemea zaidi mvua, na bima itawasaidia kupunguza hasara wanazozipata.

“Mara nyingi tumekuwa tukipata mazao tofauti na matarajio yetu kutokana na ukame na mvua chache tunazozipata hapa kwetu ,tunaomba serikalii fedha inazopata kutoka COP iwekeze zaidi katika uvunaji wa maji ya mvua yatatusaidia sana kipindi cha ukame.” Walisema Agustino na Samweli wakulima kutoka Bahi.

Kuhusu bima kwa wakulima watakao athiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa wanasema itawasaidia wasipoteze kila kitu ,huku wakisisitiza wakulima kusajiliwa kwenye mfumo ilikuweka uwazi na kuwatumia maafisa Ugani.

“Bima itatusaidia kurejesha hasara ambazo tunazipata ili kuhakikisha wakulima wote tunanufaika na bima hiyo ni muhimu serikali itusajili kuwasajili kwenye Mifumo rasmi, kwa kushirikiana na maafisa ugani waliopo katika maeneo yetu itasaidia bima kutolewa kwa uwazi na bila upendeleo, ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe,” wamesisitiza.

Miongozo ya Kimataifa
Kwa mujibu wa ripoti za Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), maeneo kame kama Dodoma yanahitaji uwekezaji wa haraka katika miundombinu ya kuhifadhi maji kama sehemu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ripoti hizo zinatambua uvunaji wa maji ya mvua kuwa hatua ya msingi ya kuongeza ustahimilivu wa kilimo katika nchi zinazotegemea mvua.

Aidha, kupitia Sharm el-Sheikh Joint Work on Agriculture and Food Security, Makubaliano ya UNFCCC yanazitaka nchi kuingiza miradi ya uvunaji wa maji katika Mipango ya Kitaifa ya Kukabiliana na Tabianchi (NAPs), ikiwemo ujenzi wa mabwawa madogo na matanki ya kuhifadhi maji kwa matumizi ya wakulima.

Kwa upande wa bima, taasisi za kimataifa kama Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Benki ya Dunia zinaitambua bima ya kilimo kama nguzo muhimu ya kuwalinda wakulima dhidi ya majanga ya tabianchi, hususan kupitia mifumo ya fidia inayozingatia viashiria vya mvua au ukame kwa wakulima wadogo.

Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Dkt. Richard Muyungi, amesema makubaliano ya COP30 yameweka utaratibu wa kufuatilia fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo uundwaji wa kamati maalumu za usimamizi.

“Kuanzia mwaka 2026, kila nchi itapata takribani dola milioni 20 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali,” amesema Dkt. Muyungi.

Utekelezaji wa miradi ya uvunaji wa maji ya mvua na kuanzishwa kwa bima ya kilimo unatekeleza moja kwa moja Sera ya Kilimo ya mwaka 2013, inayosisitiza uimarishaji wa miundombinu ya maji na mifumo ya kupunguza hatari kwa wakulima.

Hatua hizo pia zinaendana na Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NAP), unaotambua uvunaji wa maji ya mvua na bima ya kilimo kuwa nguzo muhimu za kulinda sekta ya kilimo dhidi ya athari za tabianchi.

No comments:

Post a Comment