WATENDAJI WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI LINDI WAJENGEWA UWEZO KUIMARISHA USALAMA BARABARANI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, January 10, 2026

WATENDAJI WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI LINDI WAJENGEWA UWEZO KUIMARISHA USALAMA BARABARANI.



Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Lindi, Mrakibu wa Polisi (SP) James Makumu, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika wilaya za Ruangwa na Nachingwea kwa lengo la kufanya ukaguzi wa kiutendaji na kuwapatia elimu askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Katika ziara hiyo, SP Makumu alizungumza na askari wa kikosi hicho akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma, nidhamu na uadilifu, huku akiwahimiza kuendelea kujifunza na kujiendeleza ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika usimamizi wa usalama barabarani mkoani Lindi.

Aidha, aliwapatia askari hao elimu kuhusu matumizi sahihi ya mifumo mbalimbali ya kisasa inayotumiwa na Kikosi cha Usalama Barabarani katika kudhibiti ajali, kufuatilia makosa ya barabarani na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia.

SP Makumu alieleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kupunguza ajali za barabarani mkoani Lindi kwa kuhakikisha askari wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo yote ya Jeshi la Polisi bila upendeleo wala uzembe.

Vilevile, aliwataka askari hao kuimarisha ukaguzi wa vyombo vya moto barabarani na kuhakikisha magari yote yanakidhi vigezo vya usalama kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari, sambamba na kutoa elimu kwa madereva, abiria pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Katika hatua nyingine, SP Makumu alisisitiza kuwa askari hawapaswi kusita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote watakaokiuka sheria na kanuni za usalama barabarani, akieleza kuwa utekelezaji thabiti wa sheria ni nguzo muhimu katika kulinda maisha ya wananchi.

Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya za Ruangwa na Nachingwea wamepongeza juhudi za uongozi wa kikosi hicho mkoani Lindi kwa kuwapatia mafunzo na elimu endelevu, wakiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu kwa maslahi ya usalama wa wananchi na taifa kwa ujumla.



No comments:

Post a Comment