MRADI WA UMEME JUA KISHAPU UKO MBIONI KUKAMILIKA- MHE SALOME MAKAMBA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, January 10, 2026

MRADI WA UMEME JUA KISHAPU UKO MBIONI KUKAMILIKA- MHE SALOME MAKAMBA


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Mradi wa Umeme unaozalishwa kwa nguvu ya Jua uliopo Kishapu, Mkoani Shinyanga, uko mbioni kukamilika ambapo jumla ya megawati 50 zinatarajiwa kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa ili kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani.

Mhe. Salome ameyasema hayo Januari 9, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya umeme mkoani Shinyanga, ukiwemo Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu, Mradi wa upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli pamoja na Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli kwenda Mkoa wa Simiyu.

Amesema kuwa hadi sasa mradi wa Umeme wa Jua Kishapu umefikia zaidi ya asilimia 89 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, ikiwa ni jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha kwa ajili ya kukuza fursa kiuchumi na maendeleo endelevu.

“Mradi huu umefikia zaidi ya asilimia 89 ya utekelezaji wake, na tunatarajia kwamba ifikapo mwishoni mwa mwezi huu tutaingiza megawati 50 kwenye Gridi ya Taifa. Huu ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na mtandao imara wa kusafirisha na kusambaza umeme,” alisisitiza Mhe. Salome.

Akizungumza katika Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli, ambao umefikia asilimia 44.32 , Naibu Waziri huyo wa Nishati amesema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utakuwa na uwezo wa kupeleka umeme katika reli ya kisasa ya SGR pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.

“Tunamshukuru na kumpongeza Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli. Kwetu sisi ni heshima kubwa kwa kuwa kituo hiki kitahudumia mradi mkubwa wa kimkakati wa SGR, sambamba na kupeleka umeme katika nchi jirani za Kenya na Uganda,” alifafanua Naibu Waziri Salome.

Akizungumzia Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Ibadakuli hadi Simiyu, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi TANESCO, Mhandisi Frank Mashalo, amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Simiyu na mikoa Jirani ambapo hadi sasa mradi umefikia asilimia 53 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli za uzalishaji na uchumi kwa wananchi wa Kishapu, wengi wao wanajishughulisha na kilimo cha pamba, ambacho kinahitaji nishati ya umeme kwa ajili ya uzalishaji.

Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 323 kwa awamu zote mbili. Mradi huo ulianza rasmi mwezi Desemba 2023 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari 2026.

No comments:

Post a Comment