
London, Uingereza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), amefungua kongamano la ngazi ya juu la East Africa Prospects 2026 lililoandaliwa na taasisi ya Eastern Africa Association (EAA) kwa kushirikiana na FTI Consulting, lililofanyika jijini London hivi karibuni.
Katika kongamano hilo, Waziri Mkumbo alitoa hotuba ya ufunguzi iliyosisitiza umuhimu wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kuimarisha uwajumui wa dhati wa kikanda katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, hususan katika sekta za miundombinu ya barabara na reli, nishati, pamoja na anga na usafirishaji. Alieleza kuwa miradi ya pamoja ya kikanda ni nguzo muhimu ya kuimarisha biashara, kuvutia uwekezaji wa muda mrefu, na kukuza maendeleo jumuishi ya wananchi wa ukanda huo.
Aidha, Waziri Mkumbo alitumia jukwaa hilo kueleza miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Tanzania kwa kushirikiana na nchi jirani, ikiwemo Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam na masoko ya ukanda wa Maziwa Makuu, pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Alisisitiza kuwa miradi hiyo inaongeza muunganisho wa kikanda, inapunguza gharama za usafirishaji, na kufungua fursa mpya za biashara, viwanda na ajira.
Akihitimisha, Waziri Mkumbo aliwahakikishia wawekezaji na wadau wa maendeleo kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, thabiti kisiasa, na yenye sera zinazotabirika, tayari kushirikiana na washirika wa kimataifa wanaoleta mitaji ya muda mrefu, teknolojia, na dhamira ya kujenga thamani ya pamoja. Alitoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki kuendeleza mshikamano wa kikanda kama nyenzo muhimu ya kubadili fursa zilizopo kuwa miradi inayotekelezeka, kukuza uchumi wa kanda, na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Kongamano la East Africa Prospects 2026 liliwakutanisha mabalozi, viongozi wa taasisi za uwekezaji, na wawakilishi wa sekta binafsi, kwa lengo la kujadili mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi wa ukanda wa Afrika Mashariki katika mwaka 2026 na kuendelea.





No comments:
Post a Comment