"AFRICA EDUCATE HER" YAZINDULIWA, WASICHANA WAPEWA NGUVU YA SAYANSI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 11, 2026

"AFRICA EDUCATE HER" YAZINDULIWA, WASICHANA WAPEWA NGUVU YA SAYANSI





Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kiuchumi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta hiyo ili kuongeza wataalamu wa kutosha na wenye ubora.
Prof. Mkenda alitoa kauli hiyo Februari 11, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi.

Alieleza kuwa sayansi ni msingi wa maendeleo kwa kuwa huongeza tija katika uzalishaji na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii kupitia tafiti na matumizi ya teknolojia.


“Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 36 ya wataalamu wa sayansi duniani ni wanawake. Tanzania tunalenga kufikia angalau asilimia 51 ya ushiriki wa wanawake katika sayansi,” amesema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kupanua fursa za elimu ya sayansi kwa kutoa ufadhili wa masomo kupitia programu ya Samia Scholarship, sambamba na kuhamasisha wanafunzi kusoma fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Sayansi Asilia (STEM).

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu ya sayansi ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani, lengo likiwa ni kuwa na wanasayansi bora na wa kutosha katika sekta zote.

Maadhimisho ya mwaka 2026 yamekwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya “Africa Educate Her” nchini Tanzania, inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wasichana na kuwapa fursa sawa za kujifunza, kubuni na kufanikiwa katika taaluma za sayansi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi MaryPrisca Mahundi, amesema wizara yake itaendelea kuhamasisha na kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sayansi kwa kuboresha sera, kuimarisha malezi bora na kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema Kamati inaendelea kushuhudia mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, akisisitiza kuwa mtoto wa kike kusoma sayansi ni fursa si tu kwa familia bali kwa Taifa kwa ujumla, kwa kuwa mwanamke ni mlezi na mhimili wa jamii.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Profesa Ladislaus Mnyone, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika tafiti na ubunifu unaowashirikisha wanawake na wasichana ili kuongeza ushindani wa Taifa katika uchumi wa maarifa.

No comments:

Post a Comment