
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 11,2026 jijini Dodoma ,wakati akitoa tamko kwa vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Breli yatakayofanyika kitaifa jijini Tanga.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG - DODOMA
Serikali imesema itaendelea kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Breli pamoja na teknolojia saidizi nyingine ili kuhakikisha watu wasioona wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa, sambamba na dhamira ya kutokumwacha mtu nyuma.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga, wakati akitoa tamko kwa vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Breli yatakayofanyika kitaifa jijini Tanga.
Amesema kuwa kila mwaka ifikapo Februari 12, dunia huadhimisha siku hiyo kwa lengo la kutambua mchango wa mfumo wa Breli ulioasisiwa na Louis Braille, ambao umewezesha mamilioni ya watu wasioona kusoma, kuandika na kupata elimu kwa usawa na wale wanaoona.
“Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hii muhimu. Kwa mwaka huu, maadhimisho yanafanyika katika Halmashauri zote nchini na kitaifa yanafanyika Mkoa wa Tanga,” amesema Nderiananga.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yameambatana na maonesho ya teknolojia na kazi za wasioona, upimaji wa elimu na ujuzi, kongamano la wadau, pamoja na shughuli za burudani na hotuba za viongozi wa Serikali na wadau wa maendeleo.
Naibu Waziri huyo amesema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, “Teknolojia ya Breli Husaidia Kuchochea Maendeleo kwa Wasioona na Ujenzi wa Taifa,” inalenga kuonesha namna Breli inavyowezesha ushiriki wa wasioona katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.
Akizungumzia jitihada za Serikali, Nderiananga amesema Tanzania imeweka mifumo madhubuti ya kisheria na kisera kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu. Miongoni mwa mifumo hiyo ni Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), pamoja na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura 183.
Ametaja pia Sheria ya Mtoto, Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kuwa zimeweka mazingira wezeshi ya ushiriki wa wasioona katika shughuli mbalimbali, ikiwemo za uchaguzi.
Katika sekta ya elimu, amesema Serikali imeendelea kutoa elimu ya msingi bila malipo, kuimarisha elimu jumuishi, kuanzisha na kuendeleza shule na vituo maalum kwa wanafunzi wasioona, pamoja na kusambaza vitabu vya Breli na teknolojia saidizi.
Aidha, walimu wamekuwa wakipatiwa mafunzo maalum ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona.
Kwa upande wa sekta ya afya, Serikali imetenga madirisha maalum ya huduma kwa watu wenye ulemavu na kuboresha upatikanaji wa huduma za uchunguzi, tiba na utengamao.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa Serikali imekamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Taarifa za Watu Wenye Ulemavu (PD-MIS) ili kuboresha upangaji na utoaji wa huduma, sambamba na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Mkakati wa Elimu Jumuishi (2021–2026) na Mkakati wa Kitaifa wa Teknolojia Saidizi (2024–2027).
Akisisitiza nafasi ya wasioona katika maendeleo ya Taifa, Nderiananga amesema jamii hiyo imeendelea kuthibitisha kuwa ni rasilimali muhimu kupitia mchango wao katika elimu, sanaa, michezo, ujuzi wa kazi na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni.
“Ushirikishwaji wao unaongeza tija, ubunifu na mshikamano wa kijamii. Kupitia teknolojia ya Breli na teknolojia saidizi, wanapata maarifa na taarifa zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa,” amesema.
Ameitaka jamii kwa ujumla, taasisi za umma na binafsi pamoja na mashirika ya kiraia kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mazingira jumuishi na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ustawi wa wasioona.
“Natoa wito kwa wananchi wote kushirikiana nasi kuhakikisha tunaleta ushiriki kamili wa watu wasioona katika maisha ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Serikali itaendelea kuthamini na kutambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa,” amesisitiza.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Breli yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza uelewa, heshima na usawa kwa watu wasioona, huku yakihamasisha matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta maendeleo endelevu nchini.

No comments:
Post a Comment