
KATIKA miaka ya karibuni, mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa tishio kubwa kwa uhakika wa chakula duniani.
Ukame wa mara kwa mara, misimu isiyotabirika ya mvua na ongezeko la joto, vimewaacha wakulima wadogo katika hatari kubwa ya njaa na umasikini.
Ndiyo maana katika mikutano ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi (COP), hususan COP30, matumizi ya mbegu himilivu yamepewa kipaumbele kama suluhisho muhimu kwa kilimo endelevu.
Kwa Tanzania, mjadala huu haukuishia kwenye majukwaa ya kimataifa pekee. Ndani ya Bunge la 13 jijini Dodoma, wabunge waliibua kwa kina suala la mbegu himilivu wakisisitiza umuhimu wake katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa wananchi.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko alihoji mkakati wa Serikali katika kuongeza upatikanaji wa mbegu za muda mfupi, hususan kipindi cha masika, ili kuwaepusha wakulima na hatari ya njaa.
Swali lake liliakisi wasiwasi wa wakulima wengi wanaokabiliwa na misimu mifupi ya mvua na ukame wa mara kwa mara.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema wizara yake inaendelea kufanya tathmini ya mwenendo wa mvua na hali ya hewa, huku ikiandaa mbegu za muda mfupi na za muda mrefu sambamba na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Kwa mujibu wa serikali, mkakati huo unalenga kuwafanya wakulima waendelee kuzalisha hata katika mazingira yasiyotabirika ya tabianchi.
Hata hivyo, bado kuna maswali mengi miongoni mwa wakulima na wadau wa kilimo, hususan kutoka katika mikoa inayokabiliwa na ukame kama Dodoma.
Wakulima wanahoji, mbegu hizo zinasambazwa kwa wakati gani, zinawafikia wakulima wangapi na zinapatikana kwa wingi unaokidhi mahitaji halisi?
Sambamba na hoja hiyo iliyojibiwa na Naibu Waziri Silinde, katika mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Dira ya Taifa ya 2050 uliowasilishwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wabunge waliendelea kuhoji ambaopo Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya alihoji kwa nini mamlaka kama Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na taasisi binafsi zinazozalisha mbegu himilivu zenye uwezo wa kustahimili ukame zisiwezeshwe zaidi kwa kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mbegu hizo kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Chakula, mazao, mbegu ni usalama wa nchi, bila mbegu bora hakuna chakula cha kutosha. Taasisi ya Mbegu (ASA) inazalisha tani 90,000 na wana hekta elfu 13,000 zinazotosha kuzalisha mbegu licha ya kutegemea mvua. tukiiwekea miundombinu ya umwagiliaji itaweza kuzalisha mbegu tani 22,000 na kuiwezesha Serikali kupata Sh. bilioni 33 na wakulima watapata mbegu bora bila kuagiza nje.” Alisema Bulaya.
Mbunge wa Makete, Festo Sanga alisisitiza kuwa sekta ya kilimo ndiyo inayoathirika zaidi kadri mvua zinavyoendelea kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Alisema ni wakati muafaka kwa Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika kilimo cha umwagiliaji ili wakulima waondokane na utegemezi wa kilimo cha mvua pekee.
“Sekta ya kilimo ni vema ikaendelea kuwezeshwa katika nchi yetu kwa kuwa inaongeza mapato. Mvua inakata kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo tukijikita kwenye kilimo cha umwagiliaji tutawasaidia wakulima kuacha kutegemea mvua.” Alisem Sanga.
Katika mkutano huo uliofanyika Belém, Brazil kuanzia Novemba 11 hadi 21, 2025, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilipendekeza matumizi ya mbegu himilivu likieleza kuwa mbegu hizi zina uwezo wa kustahimili ukame na misimu isiyotabirika, hivyo kusaidia wakulima wadogo kuongeza uzalishaji hata katika hali ya joto kali au mvua chache.
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), matumizi ya mbegu himilivu ni mojawapo ya njia muhimu za kuhakikisha familia na jamii zinapata chakula cha kutosha, huku zikisaidia nchi kama Tanzania kutimiza malengo ya COP30 kuhusu kilimo endelevu na uhakika wa chakula. Hata hivyo, shirika hilo lilionya kuwa bila usambazaji kwa wakati, uwekezaji wa kutosha na ufuatiliaji madhubuti wa utekelezaji, mikakati ya mbegu himilivu hubaki kuwa sera na kauli zisizoleta matokeo kwa wananchi.
Kwa Tanzania na nchi nyingine zinazokabiliwa na ukame, uwekezaji wa haraka katika mbegu himilivu na mifumo ya kilimo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi si hiari tena, bali ni hitaji la dharura. Hatua hizi zinaweza kuwa nguzo ya kuokoa maisha, kuimarisha uhakika wa chakula na kujenga mustakabali wa kilimo endelevu kwa vizazi vijavyo.

No comments:
Post a Comment