BALOZI KALLUA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO NCHINI CYPRUS - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 10, 2026

BALOZI KALLUA AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO NCHINI CYPRUS


Balozi wa Tanzania nchini Cyprus mwenye makazi Tel Aviv, Israel, Mhe. Alex Gabriel Kallua amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Cyprus, Mhe. Nikos Christodoulides katika hafla iliyofanyika jijini Nicosia, Februari 9, 2026.

Mhe. Kallua anakuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania kuwasilisha hati za utambulisho tangu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Jumla ya mabalozi 16 wasio wakazi, kutoka nchi mbalimbali waliwasilisha hati zao.

Katika mazungumzo yao ambayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus, Mhe. Constantinos Kombo, Rais wa Cyprus, Mhe. Christodoulides alisifia mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Cyprus. Alieleza kuwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus nchini Tanzania mwezi Julai, 2025, ilifungua ukurasa mpya wa mahusiano hayo. Aliongeza kuwa utiaji saini wa hati mbili za ushirikiano katika majadiliano ya kisiasa na utambuaji wa vyeti vya mabaharia ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano hayo.

Aliihakikishia Tanzania kuwa Cyprus iko tayari kuimarisha zaidi mahusiano na Tanzania katika sekta zote tulizokubaliana kwa manufaa ya pande zote mbili.

Aidha, Rais wa Cyprus aliwasihi Mabalozi wote kuendelea kuiunga mkono Cyprus katika jitihada zake za kutafuta amani ya kudumu na kuliunganisha taifa lake na watu wake kulingana na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Katika hotuba yake ya maandishi, Mhe. Balozi Kallua aliahidi kuanza mara moja kusimamia utekelezaji wa hati za makubaliano zilizosainiwa mwaka 2025 na kutafuta fursa mpya za ushirikiano katika sekta za uchumi wa buluu, elimu, utalii, biashara na uwekezaji.

Mhe. Balozi Kallua anatarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Cyprus; Mwenyekiti wa Bandari ya Cyprus na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa mazungumzo ya namna ya kuimarisha zaidi mahusiano haya.





No comments:

Post a Comment