
Na Shua Ndereka- OKULY BLOG, Morogoro
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma nchini (PSC), Jaji (Mst.) Hamisa Kalombola, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Tume kifedha, hali inayowezesha utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kuendesha vikao na kutoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa umma.
Jaji Kalombola ameyasema hayo, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Tume ya Utumishi wa Umma wa Mamlaka za Maji nchini, kinachoendelea mjini Morogoro, kikilenga kujadili utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, pamoja na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia rufaa na malalamiko, sambamba na uwasilishaji wa taarifa za kiutumishi kwa Tume.
Amesema kuwa, uwezeshaji huo wa kifedha umeiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, hali inayochangia kuboresha usimamizi wa utumishi wa umma na kuinua ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Aidha Jaji Kalombola amesema kuwa, kupitia vikao na mikutano mbalimbali ya kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma, Tume imebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika baadhi ya Mamlaka za Majisafi na Usimamizi wa Mazingira nchini, hali iliyoibua umuhimu wa kuitisha kikao kazi hicho.
“Tume imekuwa ikikumbana na changamoto hizi kwa muda mrefu, hivyo tukaona kuna umuhimu wa kukutana ili kujadili kwa pamoja namna ya kurekebisha hali hiyo na kusukuma mbele maendeleo ya taifa,” amesema Jaji Kalombola.
Ameongeza kuwa, ukiukwaji wa taratibu hizo husababisha baadhi ya rufaa kurejeshwa ili kusikilizwa upya, jambo linalochelewesha haki na mambo mengi ya watumishi wa umma.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma John Mbisso amesema kuwa, lengo la kikao kazi hicho ni kutoa mafunzo kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma na utekelezaji wake, kufuatia kubainika kwa ukiukwaji wa sheria hizo katika taasisi mbalimbali.
Amesema Tume imeandaa mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kushughulikia rufaa na malalamiko, hivyo kikao hicho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Wakurugenzi wa Huduma za Sheria pamoja na Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA kutoka Mamlaka za Maji ili kuujadili na kuuelewa mfumo huo.
“Mfumo huu unatumika katika kuwasilisha vielelezo vya rufaa na malalamiko kwa Tume ya Utumishi wa Umma, na pia unasaidia uwasilishaji wa taarifa za kiutumishi kwa wakati na kwa ufanisi,” amesema Mbisso.
Katika kikao hicho, mada mbalimbali zinawasilishwa ikiwemo, taratibu za kiutumishi kwa mtumishi wa umma kuanzia kuajiriwa hadi kustaafu (Haki na wajibu wa mtumishi wa umma), Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2023, pamoja na mchakato wa mashauri ya nidhamu, rufaa na malalamiko.
Hata hivyo, kikao kazi hicho cha mafunzo ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Mamlaka za Maji Tanzania, kinafanyika kwa muda wa siku nne, kuanzia Februari 9 hadi Februari 12, 2026 Manispaa ya Morogoro.





No comments:
Post a Comment