WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wajumbe wa Bodi za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini waamke na wasimamie majukumu yanayohusu sekta ya maji.
"Tukitoka hapa twende tukatimize wajibu wetu wa kusimamia masuala ya maji. Someni upya kazi za Bodi, ninyi si wasaidizi wa Wakurugenzi. Bodi inapaswa ijue jambo lao kabla hata halijafika kwa Mheshimiwa Waziri," amesisitiza.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Februari 24, 2026) wakati akizungumza na washiriki wa mkutano wa siku mbili wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji nchini unaofanyika katika hoteli ya Ngurdoto, jijini Arusha. Mkutano huo wa kitaifa unawakutanisha viongozi wakuu wa usimamizi wa Mamlaka 85 za maji nchini.
Waziri Mkuu amesema moja ya maeneo wanapaswa kusimamia ni kukomesha upotevu wa maji. “Leo bado tuna maeneo mengi yenye upotevu mkubwa wa maji. Twendeni tukakague miundombinu yetu, tukomeshe kitu kinaitwa upotevu wa maji. Kuna maeneo maji yanapelekwa lakini asilimia 50 yanaenda kwa wananchi na asilimia 50 yanapotea. Hebu tujiulize, hii asilimia 50 nayo ingeenda kwa wananchi ni lazima tungekuwa mbali kwenye suala zima la upatikanaji wa maji. Je, ingekuwa ni biashara ya mtu binafsi, tungeruhusu hali hiyo iendelee?,” amehoji Waziri Mkuu.
Dkt. Mwigulu amwelekeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aanze kwa kuwapima wajumbe wa bodi hizo wanamalizaje suala la upotevu wa maji.
Kuhusu uwepo wa watu wanaojiunganishia maji kiholela na hawalipi bili, Waziri Mkuu ameagiza watu wote wa aina hiyo wafuatiliwe. “Nendeni muwafuatilie ili walipie hayo maji,” amesisitiza.
Kuhusu utoaji huduma ya maji kwa wananchi, Waziri Mkuu amewataka watendaji wote wa sekta ya maji wajitume kuhakikisha maji yanasambaa kote nchini. "Tuelekeze nguvu kwenye maeneo watu wana shida ya maji. Mheshimiwa Waziri ulisema tumebakiza vijiji 1,575 lakini naelekeza kuwa kwenye taasisi zenye mikusanyiko ziwe na maji.”
“Kila shule hapa nchini, ya msingi au ya sekondari lazima pawe na maji. Kila zahanati na kila kituo cha afya, pawe na maji. Yanaweza kuwa ya mradi au ya kisima, mitambo tunayo. Fanyeni mapping vizuri. Tukijipanga vizuri, ndani ya mwaka mmoja tunaweza kufikia lengo la kila shule iwe na maji."
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wajumbe wa mkutano huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema zaidi ya sh. trilioni tatu zimetolewa na Serikali ili kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kupitia fedha hizo, huduma ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya vijijini imeongezeka na kufikia asilimia 85.2 huku upatikanaji wa maji mijini ukiongezeka na kufikia asilimia 92.5. “Hapa nchini kuna vijiji 12,333 na kati ya hivyo, vijiji 10,758 vimepatiwa maji na vimebakia vijiji 1,575 tu."





No comments:
Post a Comment