MKUU wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese,akizungumza wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani wa Halmashauri ya Mji Handeni, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi yaliyolenga kuwaimarisha katika masuala ya utawala bora, ufuatiliaji wa mapato na uelewa wa mipaka ya majukumu yao katika uendeshaji wa halmashauri.
Na Augusta Njoji
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Mji Handeni, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kuacha kutanguliza maslahi binafsi au ya kisiasa wanapotekeleza majukumu yao, na badala yake kuweka mbele maslahi ya wananchi na maendeleo ya halmashauri.
Nyamwese ametoa wito huo mjini Handeni wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani, yaliyolenga kuwaimarisha katika masuala ya utawala bora, ufuatiliaji wa mapato na uelewa wa mipaka ya majukumu yao katika uendeshaji wa halmashauri.
Amesisitiza kuwa serikali haitavumilia uzembe, hujuma wala vitendo vyovyote vinavyozorotesha maendeleo ya halmashauri, akiwataka madiwani kuwa macho na kutoa taarifa kwa wakati pindi wanapobaini mianya ya upotevu wa mapato.
“Tunaomba mkawe wabunifu na mzishauri halmashauri namna bora ya kuboresha na kusimamia vyanzo vya mapato. Nyie ndio mnaoishi na wananchi; mnapobaini kapu linavuja, tuambieni linavuja wapi na nani analivujisha ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Nyamwese.
Ameongeza kuwa madiwani ni macho na masikio ya serikali katika maeneo yao, hivyo wanapaswa kusimamia nidhamu ya watumishi, kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuchochea ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni, Margareth Killo, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi na uwajibikaji wa madiwani katika kuwahudumia wananchi. Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Handeni, Amiri Mwaliko, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Michael Chabai, wamesema mafunzo hayo yamewawezesha madiwani kufahamu vyema wajibu na mipaka yao, hali itakayopunguza migongano na kuongeza tija katika utendaji wa halmashauri.

No comments:
Post a Comment