KAMATI YA BUNGE YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TAMISEMI KATIKA USIMAMIZI WA ELIMU MSINGI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 12, 2026

KAMATI YA BUNGE YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TAMISEMI KATIKA USIMAMIZI WA ELIMU MSINGI NCHINI


Na OWM - TAMISEMI, Dodoma


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Florent Kyombo amesema kamati yake itashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM -TAMISEMI) katika usimamizi na uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari ili wanafunzi wapate ufaulu mzuri utakaowezesha kutimiza ndoto zao kitaaluma.

Mhe. Kyombo ametoa ahadi hiyo leo Februari 12, 2026 wakati wa kikao cha mafunzo kwa wajumbe wa kamati yake, yaliyohusu Usimamizi na Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari nchini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM), katika Ukumbi wa Anne Makinda Bungeni Jijini Dodoma.

“Mhe. Waziri wa TAMISEMI tunakuamini wewe pamoja na watendaji wa ofisi yako, hivyo sisi tunakuahidi ushirikiano ili kuiwezesha ofisi yako kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” amesisitiza Mhe. Kyombo.

Aidha, Mhe. Kyombo amesema, wajumbe wa kamati yake wamepata uelewa mzuri kuhusu Usimamizi na Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari na kuongeza kuwa, kamati yake ni jicho la TAMISEMI na ipo tayari kuendelea kutoa ushirikiano utakaowezesha usimamizi na uendeshaji mzuri wa shule za msingi na Sekondari ili ziwe na manufaa kwa taifa kwa kutoa rasilimali. watu itakayochangia kuleta maendeleo katika taifa.


Mmoja wa Wajumbe wa kamati hiyo, Mhe. Jesca Magufuli ameshukuru kwa kupatiwa mafunzo ambayo yamewapa uelewa wa kutofautisha majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Wizara ya Elimu kwenye sekta ya elimu, kwani awali yeye binafsi alikuwa na changamoto ya kutofautisha majukumu ya ofisi hizo.


Naye, Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Mhe. Mwantatu Khamisi ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kwa kuboresha miundombinu ya elimu ili kuwawesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanapata elimu katika mazingira mazuri.

Mhe. Hawa Mwaifunga ni mjumbe mwingine wa kamati hiyo ambaye amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kujenga miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora ni si bora elimu, na kuongeza kuwa katika jimbo lake Mhe. Rais amepeleka zaidi ya Shilingi Bilioni 2.1 kwa ajili ya kuongeza madarasa katika shule zenye wanafunzi wengi.


Akizungumza kuhusu elimu ya lazima, mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Lucy Mwakyembe amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassana kwa maono yake ya kuwa na elimu ya lazima ya miaka 10 ambayo inajumuisha darasa la kwanza hadi la sita na kidato cha kwanza hadi cha nne.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Jafari Chege ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kutoa fedha zaidi ya Shilingi Milioni 275 kwa ajili ya kukarabati shule moja jimboni kwake, na kuongeza kuwa fedha hizo zimewezesha kukarabati shule hiyo na kujenga shule nyingine mpya ya msingi.


Akizungumzia stahiki za walimu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika kuhakikisha walimu wanapata stahiki zao ikiwemo upandishwaji vyeo na malipo ya malimbikizo ya mishahara pamoja na fedha za likizo, na ameahidi kuendelea kufanyia kazi suala la msawazo wa walimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – UTUMISHI.

No comments:

Post a Comment