BoT YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA FEDHA KAMA SHADA LA MAUA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 12, 2026

BoT YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA FEDHA KAMA SHADA LA MAUA


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amewaonya wananchi wanaozifunga fedha kama shada la maua kwa ajili ya zawadi kwa wapendwa wao, hususan katika kipindi hiki cha msimu wa Sikukuu ya Wapendanao (Valentine).

Akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika leo Alhamisi, Februari 12, 2026, ofisini kwake jijini Dodoma, Gavana Tutuba amesema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria na husababisha uharibifu wa fedha.

Amesema kuwa fedha ni tunu ya Taifa, na utaratibu wa kuziweka katika mashada ya maua mara nyingi huhusisha kubandikwa kwa gundi pamoja na kukunjwa, hali inayochangia kuchakaa kwa haraka au kuchanika. Kutokana na uharibifu huo, Benki Kuu hulazimika kuchapisha fedha mpya mara kwa mara, jambo linaloongeza gharama kwa Taifa.

“Hizi fedha tunazichapisha kwa gharama kubwa. Zinapobandikwa gundi na kukunjwa hovyo zinachakaa mapema, hivyo BoT inalazimika kuchapisha fedha mara kwa mara. Kama unataka kumpa zawadi ya Valentine mpendwa wako, mnunulie bidhaa yenye thamani au mpatie fedha hizo zikiwa katika hali yake ya kawaida,” amesema Gavana Tutuba.


Aidha, Gavana Tutuba amesisitiza kuwa kila anayeshika fedha ya Tanzania ana wajibu wa kuzitunza na kuzihifadhi, kwa kuwa ni miongoni mwa alama na tunu muhimu za Taifa.

No comments:

Post a Comment