
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi, Dkt. Charles Msonde ameitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kuendelea kuimarisha uwajibikaji, matumizi sahihi ya rasilimali, mifumo ya udhibiti wa ndani pamoja na mageuzi ya kidijitali ili kuboresha huduma na kuongeza mapato ya Taasisi.
Hayo ameyasema Naibu Katibu Mkuu huyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la 13 la Wafanyakazi wa Bodi hiyo jijini Dodoma na kusisitiza kuongeza ubunifu na ufanisi ili kuifanya Bodi kuwa ya pekee.
“Ipo haja ya kujiuliza kutokana na taaluma mliyonayo mnaitumiaje, ni lazima kuhakikisha siku zote mnapandisha weledi wenu na kuwa wa kipekee kujulikana katika Taifa letu kupitia miradi mnayoibuni”, amesema Dkt. Msonde.
Dkt. Msonde amewataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, weledi na mshikamano na kufafanua kuwa mafanikio ya Bodi hiyo yanategemea ushirikiano wa watumishi hao.
Ametoa rai kwa menenejimenti ya Bodi hiyo kutumia changamoto wanazokutana nazo katika utendaji wao na majukumu yao ya kila siku kama fursa ili kuwezesha umoja na mshikamano wa Taasisi.
Aidha, Dkt. Msonde amelitaka Baraza la Wafanyakazi na TAMICO kuendelea kuwa daraja la kujenga na si kubomoa kati ya watumishi na Menejimenti.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa AQRB, Mbunifu Majengo, Dkt. Daniel Matondo ametaja mafanikio ya Bodi hiyo ikiwemo utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya udhibiti wa wataalam, kampuni za ushauri pamoja na kusajili na kukagua miradi.
Naye, Katibu Mkuu wa TAMICO Taifa, Partenus Rwechungura amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi ikiwa ni nguzo ya kuleta maendeleo katika Taasisi hiyo.





No comments:
Post a Comment