
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka Makatibu Wakuu wa Wizara hiyo kushirikiana kikamilifu katika kutafuta vyanzo vipya vya nishati ya umeme ili kufikia uzalishaji wa megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 ambapo kwa sasa tumefikia takribani megawati 4,400.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo leo Februari 12, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam wakati akimpokea Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mapema wiki hii.
Amesema uteuzi huo unaonesha imani kubwa ya Rais kwa viongozi hao, na kumpongeza Mhandisi Felchesmi Mramba kwa kuteuliwa tena kuendelea kushika nafasi ya Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu.
“Sina mashaka na wewe, naamini utaendelea kuitendea haki nafasi hiyo na kusimamia vyema miradi ya umeme na nishati jadidifu,” amesema Mhe. Ndejembi.
Aidha, amempongeza Dkt. Mataragio kwa kupandishwa cheo kutoka Naibu Katibu Mkuu hadi Katibu Mkuu anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia na kumtaka kutumia mamlaka yake mpya kuharakisha utekelezaji wa masuala yaliyokuwa yakikwama katika sekta hiyo.
Amesema Serikali imelenga kufikia uzalishaji wa megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi, hivyo ni muhimu viongozi hao kuunganisha nguvu katika kutafuta na kuendeleza vyanzo vipya vya nishati ya umeme.
Pia amewataka viongozi hao kutembelea miradi mara kwa mara badala ya kukaa ofisini ili kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya umeme, gesi na mafuta, kwa lengo la kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za nishati.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, amemshukuru Rais kwa kuendelea kumuamini na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha miradi ya umeme inatekelezwa kwa ufanisi na upatikanaji wa umeme unakuwa wa uhakika nchini.
Naye, Katibu Mkuu anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amemshukuru Rais kwa uteuzi huo na kuahidi kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za mafuta na gesi asilia.
Amesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni kuhakikisha mradi wa uchakataji wa gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) unaanza kutekelezwa, kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi majumbani, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya kutosha na ya uhakika.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Mhe. Rais Samia alifanya maboresho ya muundo wa Wizara ya Nishati kwa kuteua Makatibu Wakuu wawili, ambapo Mhandisi Mramba ameendelea na wadhifa wake wa kushughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, huku Dkt.Mataragio akiteuliwa kushughulikia Mafuta na Gesi Asilia.



No comments:
Post a Comment