MAAFISA TAMISEMI WAJENGEWA UWEZO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI INAYOZINGATIA MATOKEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 24, 2026

MAAFISA TAMISEMI WAJENGEWA UWEZO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI INAYOZINGATIA MATOKEO



Na Shua Ndereka, OKULY BLOG - Morogoro


Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) wamepatiwa mafunzo juu ya Ufuatiliaji na Tathmini inayozingatia Matokeo, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kusimamia mipango na uwekezaji wa umma unaozingatia matokeo.

Mafunzo hayo yamefanyika hivi karibuni kwa muda wa siku nne mjini Morogoro, yakijikita katika Ufuatiliaji na Tathmini Unaozingatia Matokeo (Result Based Monitoring and Evaluation – RBME), na kuashiria hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa taasisi kusimamia mipango na uwekezaji wa umma unaolenga matokeo.

Mafunzo yamewezeshwa kupitia Msaada wa Kiufundi wa Mpango wa SASA unaotekelezwa na DAI Global, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na nchi nne wanachama wake ambazo ni Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji na Denmark, chini ya mwavuli wa Timu Ulaya.

Mpango wa SASA unatekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Halmashauri ya Jiji la Tanga, pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kisiwani Pemba, ukilenga kuboresha utawala wa mijini, kuimarisha ustahimilivu wa miji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa ndani.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Bw. Ulrick Jorgensen, amesema kuwa kupitia maeneo yote ya mradi, wataboresha huduma na miundombinu ya umma na kuhakikisha inadumu ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

“Tunahusiana na taasisi kadhaa za maeneo husika, ikiwemo sekta binafsi na mamlaka za serikali za mitaa, tutashirikiana kwa karibu na wadau wote kujaribu kuunda miradi ya uwekezaji itakayochangia kufanikisha malengo ya programu,” amesema Jorgensen.

Ameongeza kuwa, wanataka matokeo ya programu yafuatiliwe ili kuwezesha maamuzi yanayotokana na taarifa sahihi, kwa kuona kinachofanya kazi na kisichofanya kazi, hivyo serikali iweze kuwekeza rasilimali zake kwenye shughuli zenye tija na kurekebisha zile zisizofanikiwa ipasavyo.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha mifumo ya usimamizi wa utendaji katika taasisi za umma na kwa wadau wote, ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatafsiriwa kuwa matokeo ya maendeleo yanayopimika na endelevu.

Naye Saphinael Mapesa, Mchumi Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, amesema maafisa wamejifunza umuhimu wa kufanya tathmini za utayari, zinazosaidia taasisi kubaini kama zina mifumo, uwezo na michakato muhimu ya kuanzisha na kuendeleza mfumo wa RBME.

Amesema lengo kuu la mafunzo ni kuimarisha ufuatiliaji na tathmini inayozingatia matokeo, ambapo maafisa wamewezeshwa kupanga mipango inayozingatia matokeo, kuhakikisha mipango inaleta matokeo tarajiwa zaidi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli pekee.

“Mafunzo yamesisitiza umuhimu wa kutumia matokeo kwa ufanisi, kwa kujifunza kutafsiri na kutumia ripoti, washiriki wamehimizwa kuanzisha utamaduni wa kitaasisi wa kujifunza na kurekebisha mbinu kulingana na ushahidi na uzoefu wa awali. Hili linaimarisha uwajibikaji kwa umma na kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Mapesa.

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA, Innocent Mrema, ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, amesema mafunzo yamewaongezea ujuzi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, hususan katika mifumo wanayoisimamia ndani ya TAMISEMI.

Aidha, maafisa walijifunza aina mbalimbali za ufuatiliaji na tathmini, wakibaini tofauti kati ya ufuatiliaji wa utekelezaji na ufuatiliaji wa matokeo, pamoja na namna vipengele hivyo vinavyosaidiana ndani ya mfumo thabiti wa usimamizi wa utendaji.

Vilevile, washiriki walipatiwa uelewa kuhusu aina tofauti za tathmini, madhumuni yake na namna ya kuandaa mipango ya tathmini kwa vitendo vinavyoarifu ufanyaji maamuzi na uboreshaji wa sera.

Pia Mafunzo yalisisitiza umuhimu wa kubadilisha takwimu kuwa taarifa zenye maana zinazoonesha hali ya miradi, programu na sera, kubaini changamoto na kuunda fursa za maboresho kwa wakati muafaka.

Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa uendelevu wa mifumo ya RBME ndani ya OWM- TAMISEMI na katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhakikisha kuwa ufuatiliaji unaozingatia matokeo unaingizwa katika utendaji wa kila siku badala ya kubaki kuwa mpango wa mara moja.

Wakati Tanzania ikiendelea kuweka vipaumbele katika utoaji wa huduma bora na utawala unaowajibika, mafunzo ya RBME yanayotolewa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo yanaonesha dhamira ya dhati ya kujenga mifumo inayopima matokeo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi.





No comments:

Post a Comment