
Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekutana na Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Tone Tinnes na kufanya mazungumzo ya namna ya kuboresha ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kuikinga jamii dhidi ya majanga yanayoweza kuwakumba kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Prof. Shemdoe amekutana na Balozi Tinnes leo Februari 05, 2026 Jijini Dodoma katika ofisi ndogo za Wizara na kujadiliana masuala mbalimbali ili kuimarisha mahusiano ya kiutendaji baina ya OWM-TAMISEMI na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
Katika mzungumzo hayo wamekubaliana kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuwezezesha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika sekta za afya na elimu msingi, miundombinu ya barabara na huduma nyinginezo za kijamii, ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha, Prof. Shemdoe ameishukuru Serikali ya Norway kwakuwa mmoja wa wadau wa maendeleo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuiomba nchi hiyo kuendelea kuchangia maendeleo nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya Watanzania.
Kwa upande wake, Balozi wa Norway nchini Tanzania Mhe. Tinnes ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Norway na Tanzania, ushirikiano ambao una tija katika maendeleo ya wananchi.
Katika kikao hicho, Balozi huyo wa6 Norway aliambatana na Msaidizi wake Dkt. Lutgart Lenaerts pamoja na Mshauri Mwandamizi Dkt. Yassin Mkwizu.

No comments:
Post a Comment