VETA YAWARASIMISHA MAFUNDI 25,523, YALENGA KUFIKIA 80,000 IFIKAPO 2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, February 16, 2026

VETA YAWARASIMISHA MAFUNDI 25,523, YALENGA KUFIKIA 80,000 IFIKAPO 2027



Na Okuly Julius, OKULY BLOG - DODOMA


Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inaendelea kutekeleza Programu ya “Mama Samia na Urasimishaji Ujuzi” inayolenga kuwatambua rasmi mafundi na vijana waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi wa mafunzo ili kuwawezesha kupata vyeti vinavyotambulika, ajira na fursa za zabuni za Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Mzee Kasore, amesema mamlaka hiyo imejipanga kuwafikia mafundi waliopo mitaani na katika maeneo ya kazi ili kuwapima na kuwatunuku vyeti kupitia mpango wa Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (Recognition of Prior Learning – RPL).

“Kuna mafundi wengi wazuri wanaofanya kazi kwa ufanisi mkubwa lakini hawana vyeti vinavyotambulika rasmi. Sisi kama VETA tutawafuata walipo ili kuwarasimisha na kuwapatia vyeti vitakavyowasaidia kupata ajira na zabuni mbalimbali,” amesema CPA Kasore.

Amesema hadi kufikia Januari 2026, jumla ya wanagenzi 25,523 (wanaume 21,547 na wanawake 3,976) wamenufaika na mpango huo. Katika mwaka wa fedha 2025/2026, VETA imelenga kurasimisha mafundi 30,000 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu inayolenga kufikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027.

Mbali na urasimishaji ujuzi, VETA pia inaendesha Mpango wa Mafunzo Jumuishi ya Kukuza Ujasiriamali kwenye Sekta Isiyo Rasmi (Integrated Training for Entrepreneurship Promotion – INTEP) unaolenga kuwaongezea ujuzi vijana na wanawake wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi zisizo rasmi kama mama na baba lishe, mafundi nguo, seremala na wasindikaji.

Kupitia mpango huo, washiriki hupewa mafunzo ya kuboresha uzalishaji na kuongeza tija. Hadi Januari 2026, jumla ya wajasiriamali 7,040 wamenufaika, huku VETA ikipanga kutoa mafunzo kwa vijana na wanawake 2,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.

VETA kwa kushirikiana na AGRA Tanzania na taasisi nyingine, inatekeleza Mradi wa Ujasiriamali wa Vijana kwa Mustakabali wa Chakula na Kilimo (YEFFA) unaotarajiwa kuwanufaisha vijana 5,631 kutoka mikoa 19 kwa mafunzo ya muda mfupi katika stadi za kilimo na teknolojia.

Aidha, kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), VETA inatekeleza Mradi wa Timiza Malengo unaolenga kuwawezesha wasichana walio katika hatari ya maambukizi ya VVU kupitia mafunzo ya ufundi stadi na stadi za maisha. Hadi sasa wasichana 2,269 wamehitimu, huku 2,771 wakitarajiwa kuendelea na mafunzo ili kufikia lengo la wanufaika 5,040 ifikapo Desemba 2026.

Miradi ya Wezesha Binti na Inclu-Cities inayofadhiliwa na Enabel pia inalenga kuwanufaisha vijana 1,400 ifikapo 2028, ambapo hadi sasa vijana 531 wamenufaika.

CPA Kasore amewataka vijana na wanawake waliopo katika vikundi vya ujasiriamali kuwasilisha maombi kupitia ofisi za kanda za VETA ili kunufaika na fursa za mafunzo zinazotolewa.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri, kuajirika na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment