WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, February 16, 2026

WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumatatu (Februari 16, 2026) amekagua mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani mkoani Tanga na amesema kuwa amefurahishwa na utekelezaji wake.
Amesema kuwa mradi huo ni wa kimkakati ambao utagharimu Dola za Marekani bilioni 5.65 ni kielelezo cha undugu kati ya Tanzania na Uganda. “Ninatambua msisitizo uliowekwa na viongozi wetu, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Miseveni katika utekelezaji wa mradi huu.”
 
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ambaye yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka uzito unaostahili katika kutekeleza mradi huo ambao umefikia asilimia 81 ya utekelezaji kwa heshima ya undugu kati ya Tanzania na Uganda.
 
“Lakini tutaendelea kuweka uzito unaostahili kwa heshima ya kulinda uhuru wetu kwa kuwa ni nchi huru ambayo inaweza kujitegemea kutekeleza mradi wa kiwango hiki, hiki ni kielelezo kwamba nchi yetu inaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mikubwa ya maendeleo.”
 
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amewatahadharisha watu wanaoanzisha makampuni na kuyaita ya wazawa huku yakiwa yanamilikiwa na wageni ili kunufaika na fursa ya ‘Local Content’ ya Ushirikishwaji wa Watanzania mradi kwamba watakaogundulika watafungiwa na hawatafanya kazi tena nchini.
 
“Wapo wasio waaminifu wanawatumia Watanzania kuanzisha makampuni wanasema ni ya wazawa. Tunataka kuinua kampuni za Watanzania, upo mchezo mgeni anatumia anuani ya Mtanzania ambaye si mnufaika, wale watakaogundulika wanafanya ujanja tutawafungia na hawatafanya kazi tena kwetu.”
 
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa kufanya hivyo ni kuwatapeli Watanzania na kuwaibia fursa. “Tumekupa mradi una nafasi yako tena asilimia kubwa, tunataka hiyo sehemu ndogo inawanufaishe Watanzania na ninyi mnawaibia, wale tuliowapa kazi ya kufuatilia hili tukigundua upo huu mchezo tutakuchukulia hatua kwa kuwa tutajua na wewe ni sehemu yao.” Amesema Mheshimiwa Dkt. Nchemba
 
Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameagiza wasimamizi wa mradi huo wahakikishe kuwa baada ya ujenzi huo kukamilika kipaumbele cha ajira kitolewe kwa wale waliofanya kazi kwenye mradi huo kwa kuwa wanakidhi vigezo.
 
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema kuwa mradi huo ambao ulianza utekelezaji wake mwaka 2022 na unategemea kukamilika ifikapo Julai 2026 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanahisa kwa asilimia 15.

No comments:

Post a Comment