
Na Mwandishi wetu, Tanga.
Je umewahi kutembelea Mapango ya Amboni na kupata simulizi zake?
Pengine kwa muda mrefu unatafuta mchumba uoe au uolewe lakini mambo kila ukiyapanga hayakai mkao ulionyooka, suluhisho la jambo hili linapatikana kwa kutembelea mapango ya Amboni Tanga ili uweze kufanikisha lengo lako kupitia pango linaloitwa Fatuma.
Hifadhi ya Mapango ya Amboni ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yana maajabu mengi lakini mojawapo ni uwepo wa pango la Fatuma linalotumiwa na wageni mbalimbali ambao wana shida zinazowatatiza ikiwemo suala zima la mtu kukwama kutokuoa au kuolewa.
Muongoza watalii katika mapango hayo Muhsini Juma anaeleza kuwa watu wengi wamekuwa wakifanikiwa kupata wenza wao wanapofika katika pango la Fatuma ambalo limekuwa likitumika toka enzi za mababu kwa watu mbalimbali kufika na kuomba kupata mume au mke kwa kuishi nae kama mume na mke
“Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na changamoto sana ya vijana kupata wake au waume wa kuwaoa, lakini wakifika katika pango hili na kusema nia yao na kutambika basi wanafanikiwa na kumekuwa na shuhuda nyingi za wadau ambao wamefanikisha jambo hilo na kurudi kutupa mrejesho”,alisema Muhsin.
Umaarufu wa pango hili umewafanya wageni kwa nyakati tofauti kutembelea na kujifunza jinsi ya kufanya matambiko hayo na baada ya muda si mrefu basi baadhi hurudi kwa ajili ya shukran na inaaminika kwamba si wenyeji tu wa mkoa wa Tanga wanaotembelea mahali hapo bali pia na watu katika maeneo mengine nje ya nchi.
Muhsin anaeleza kuwa ukifika katika pango la Fatuma kama una mtu ambaye unataka kumuoa au kukuoa basi unataja jina lake na kumuita na haitochukua muda mrefu mtu huyo mwenyewe ataanza kukutafuta kwa lengo la kutaka kuoa au kuolewa.
Na kwa wale ambao hawana mtu kabisa wakifika katika mapango hayo wanachotakiwa kusema ni kwamba mimi mwaka huu nataka kuoa au kuolewa na namkusudia mtu flani, mwenye sifa Fulani... haichukui muda mrefu wanapata wenza wa kufunga nao ndoa.
Pango hili la Fatuma ambalo ni miongoni mwa mapango yaliyopo Amboni pia linatumika kwa kufanya matambiko yanayohusu masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kupata mtoto, kuombea mvua inyeshe, kupata kazi na mambo mengine na ndiyo maana ukifika katika pango hilo watu kadhaa wa kadhaa hufanya maombi yao na mara nyingi hawataki waonekane zaidi ya kufuata taratibu za wenyeji wao kw autulivu na faragha.
Yassin anasimulia kuwa Pango la fatuma halitaki mtu ambaye ametoka kufanya mapenzi akaingia pango hilo bila kuoga kwa kuwa anaweza kupata matatizo au mikosi.
Mwanaume akiingia kwenye pango hilo bila kuoga kuna uwezekano wa kishndwa kufanya tendo la ndoa hadi hapo atakapokwenda kwa Wazee wa kimila na kusaidiwa na hivyohivyo kwa mwanamke akiingia bila kuoga kama ametoka kufanya mapenzi, mfumo wa mzunguko wa hedhi unaweza kuongeza siku tofauti na mzunguko za mwanzo aliouzoea.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeweka utaratibu mahsusi wa kuhakikisha kuwa jamii ya mkoa wa Tanga na wale ambao bado wanaamini mambo hayo wanapata wasaa wa kufanya matambiko yao bila kuathiri utamaduni huo uliopo miaka na miaka.
Hayo ndiyo maajabu ya pango la Fatuma na hii inadhihirisha kwamba mwenda tezi na omo marejeo ngamani, Amboni ndiyo ngama yako ya kupata mume au mke ,usidharau mila kwani mdharau mila ni mtumwa.


No comments:
Post a Comment