‎WAZIRI DKT. GWAJIMA ASISITIZA USHIRIKIANO WA JAMII KUTOKOMEZA UKEKETAJI NA KUIMARISHA MALEZI YA MTOTO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 11, 2026

‎WAZIRI DKT. GWAJIMA ASISITIZA USHIRIKIANO WA JAMII KUTOKOMEZA UKEKETAJI NA KUIMARISHA MALEZI YA MTOTO


‎Na WMJJWM – Arusha

‎Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa jamii kushirikiana kikamilifu na Serikali katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji wa wanawake na wasichana, akibainisha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, mikoa ya Arusha na Manyara bado ina viwango vya juu vya ukeketaji. akisisitiza kuwa mapambano hayo hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa viongozi wa dini, wazazi, wazee wa mila, vijana na mashirika ya kiraia.
‎Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Shirika la Compassion International Tanzania wilayani Monduli,Mkoa wa Ausha katika kata ya Sepeko Dkt. Gwajima amelipongeza shirika hilo kwa uwekezaji wake kwa watoto na vijana kupitia elimu, afya, malezi bora na uwezeshaji wa kiuchumi kwa familia. Alieleza kuwa uwekezaji kwa mtoto ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa taifa, huku Serikali ikiendelea kuthamini mchango wa shirika hilo unaowafikia watoto zaidi ya 120,000 katika mikoa 22 nchini.
‎Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa kampeni ya “Mtoto ni Malezi”, akibainisha kuwa malezi chanya ndani ya familia ni msingi wa kuzuia ukatili dhidi ya watoto, mimba na ndoa za utotoni pamoja na mmomonyoko wa maadili. Amewakumbusha wazazi na walezi kuwa jukumu la malezi linaanzia nyumbani na kuonya dhidi ya kuwaacha watoto kulelewa na mitandao, simu au mazingira yasiyo salama.
‎Aidha, Dkt. Gwajima ameagiza viongozi wa wilaya na halmashauri kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, akisisitiza kuwa ustawi wa jamii hauwezi kufikiwa bila huduma bora za kijamii huku akihimiza jamii kuendelea kupaza sauti dhidi ya ukeketaji kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka 2026, “Sauti Yetu; Tokomeza Ukeketaji.”
‎Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mheshimiwa Gloriana Kimath, amepongeza Wizara na Shirika la Compassion International Tanzania kwa utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, akieleza kuwa imechangia kuimarisha ustawi wa jamii, kupunguza umaskini wa kaya na kusaidia mapambano dhidi ya ukatili wa watoto, hususan ukeketaji na ndoa za utotoni huku akiahidi kufanyia kazi na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo
‎Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Compassion International Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mary John Kasanga amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuwahudumia watoto na vijana kupitia malezi chanya na uwezeshaji wa familia kiuchumi, sambamba na kuunga mkono kampeni ya “Mtoto ni Malezi” na juhudi za kitaifa za kutokomeza ukeketaji.

No comments:

Post a Comment