WAZIRI MKUU ACHUKIZWA NA MIGOGORO YA ARDHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 6, 2026

WAZIRI MKUU ACHUKIZWA NA MIGOGORO YA ARDHI



WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewasisitiza Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na watumishi wa umma wahakikishe wanatenga muda wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao hususani kwenye migogoro ya ardhi katika ngazi zao za kiutawala.

Ameyasema hayo leo Ijumaa, Februari 6, 2026 wakati wa kuahirisha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 jijini Dodoma, akisisitiza kuwa viongozi hao wanapaswa kuwafuata wananchi, kuwasikiliza na kuchukua hatua za haraka za kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakiwa katika maeneo yao.

“Wafuateni, wasikilizeni na tatueni kero zao ili wasilazimike kwenda ngazi za juu au kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa kwa masuala ambayo mngeweza kuyafanyia kazi.” Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wananchi wakihudumiwa ipasavyo.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa upatikanaji wa elimu bora katika ngazi mbalimbali, lengo likiwa ni kuwawezesha wanafunzi wa Kitanzania kupata ujuzi utakaomudu ushindani Kitaifa na Kimataifa.

Waziri Mkuu amesema kuwa mbali na upatikanaji wa elimu bora Serikali imepata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuzindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unaolenga kuhakikisha mtoto wa darasa la tatu anasoma, anaandika na anahesabu bila shida.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imeajiri na kuwapangia vituo vya kazi jumla ya walimu 7,000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati na kukamilisha mpango wa pamoja kati ya Waajiri, Vyuo vya Ufundi Stadi na Vyuo Vikuu kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji ya sekta za kipaumbele.

Amesema kuwa Serikali imeimarisha matumizi ya TEHAMA shuleni kwa kusambaza vifaa katika shule za msingi na sekondari na kuendeleza tafiti na bunifu kupitia mfuko maalum wa Samia Commercialization Fund ili kubidhaisha bunifu na Teknolojia.

No comments:

Post a Comment