WAZIRI MKUU AAGIZA FAGIO LIPITE MUHEZA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 18, 2026

WAZIRI MKUU AAGIZA FAGIO LIPITE MUHEZA


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Waziri wa Nchi (OWM – TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe arudi Halmashauri ya Muheza na kusafisha watumishi wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za mradi wa jengo la ofisi.

Ametoa agizo hilo jana (Jumanne, Februari 17, 2026) wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mkoa wa Tanga katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani humo yaliyofanyika kwenye Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

“Muheza ndiyo wilaya iliyonidisappoint sana kwa sababu huku kwingine nimekuta upungufu bali kule Muheza ni uharibifu. Mheshimiwa Waziri kesho rudi Muheza, nenda kachukue hatua. Shirikiana na Waziri wa Utumishi, mchukue hatua,” alisisitiza.

Dkt. Mwigulu amesema kuna baadhi ya vifaa vilinunuliwa lakini havikufika site (eneo la mradi). “Nondo zenye thamani ya shilingi milioni 9.2 zililipwa kwa mzabuni Saifi Store wa Tanga lakini hazikufikishwa site, maana yake zimechepushwa.”

“Kuna marine boards vipande 192 vyenye thamani ya shilingi milioni 7.8 havikufika site. Wanaohusika ni Mhasibu, Rajab Mushi na Mhandisi Abdalla Jaha na Afisa anayehusika kupokea vifaa.”

Alisema mbali ya hivyo, kuna malipo mengine ya sh. milioni 4.4 yalifanywa ili kulipia mifuko 3,800 ya saruji lakini mifuko 300 haikufika kwenye eneo la ujenzi. “Afisa manunuzi na Afisa utumishi ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya mapokezi ya vifaa vya mradi watafutwe hawa pamoja na Mkurugenzi wa Mwanambonde General Enterprises.”

Waziri Mkuu alisema kuna ukiukwaji wa taratibu za serikali ambao ulifanyika ikiwemo kumlipa mshauri mwelekezi bila ya kuwa na mkataba wowote. “Kuna huyu AG Engineering amelipwa shilingi milioni 98.7 bila kuwa na mkataba. Huyu kalipwa za nini? Kuna mshauri mwelekezi kalipwa shilingi milioni 11.9 bila mkataba.”

“Kibaya zaidi, shilingi milioni 343 zimetumika nje ya mradi kwa kulipana posho. Mheshimiwa Waziri nenda kasafishe wote pale. Safisha wote pale hii wilaya ianze upya. Ongea na Waziri wa Utumishi kila mmoja apate adhabu anayostahili,” alisisitiza.

Kwa ujumla, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mkoa huo wakamilishe hoja za sekta mbalimbali zilizoibuliwa na wananchi kwenye wilaya na Halmashauri zote alizopita. “Wakuu wa Wilaya wafanye ziara katika kata na kusikiliza kero za wananchi. Wao wanataka kusikia majibu ya serikali. Wanataka jambo lao litatuliwe na serikali.”

Mapema, Mkuu wa Mkoa Tanga, Dkt. Batilda Burian alimshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara kwenye wilaya zote saba za mkoa huo, Halmashauri 11 na majimbo 12 ambako alikagua na kuzindua miradi yenye thamani ya sh. bilioni 751.

“Ziara yako ni darasa ambalo limetupa namna mpya ya kuwatumikia wananchi. Sisi tunabaki na kauli yako kwamba tusizoee matatizo ya wananchi, tutaifanyia kazi kwa kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi,” alisema.

No comments:

Post a Comment