BILIONI 20.26 ZA MRADI WA TACTIC KULETA MAPINDUZI YA MIUNDOMBINU IRINGA MJINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 20, 2026

BILIONI 20.26 ZA MRADI WA TACTIC KULETA MAPINDUZI YA MIUNDOMBINU IRINGA MJINI


‎Na Mwandishi Wetu - Iringa

‎Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ni miongoni mwa miji inayonufaika na utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) ambapo miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara na soko la kisasa vitatekelezwa.
‎Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bi. Happiness Nnko alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu hali ya utekelezaji wa mradi huo kwa Manispaa ya Iringa.
‎Ameeleza kuwa katika Manispaa hiyo miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 5.3, ujenzi wa soko la kisasa pamoja na ujenzi wa jengo la usimamizi wa mradi ambalo litatumika kama jengo la wahandisi ambapo kwa ujumla mradi huo utagharimu shilingi Bilioni 20.26.
‎"Nitumie fursa hii kuipongeza serikali kwa ujio wa mradi huu katika Manispaa yetu, moja ya faida za mradi huu ni kukuza uchumi wa hapa kwa mfano soko la zamani lilikuwa na wafanyabiashara takribani 70 lakini baada ya kukamilika kwa soko la kisasa watafika 150", amesema Bi. Happiness
‎Aidha, ameeleza kuwa licha ya barabara kurahisisha shughuli za usafiri pia zitasaidia katika kuongeza thamani ya viwanja katika maeneo mbalimbali
‎Kwa upande wake, Meneja wa Wakala ya  Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ambaye pia ni Mratibu mwenza wa mradi huo Mhandisi Barnaba Jabir amesema kuwa mradi huo upo katika hatua ya utekelezaji na kuahidi kuwa usimamizi utafanyika kwa kina ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi. 
‎" Mradi huu umeanza na upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, usimamizi wa kutosha unafanyika ili malengo ya serikali yaweze kutimia", amesema Mhandisi Barnaba.
‎Naye, Mhe. Hossea Kabelege Diwani wa Kata ya Kihesa amesema kuwa kuanza kwa mradi huo kumepelekea kuongezeka kwa ajira lakini pia mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuongezeka baada ya kukamilika kwa mradi huo. 
‎Bw. Edwin Mvera mkazi wa Manispaa ya Iringa amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya mawasiliano kati ya kata moja na nyingine hasa kipindi cha masika na kwamba kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kutasaidia wananchi kusafiri kwa urahisi na shughuli za kiuchumi kukua.
‎"Tunaishukuru serikali kwa kuleta mradi huu kwani baada ya kukamilika, mawasiliano yataboreshwa na thamani ya ardhi itapanda na kwa ujumla uchumi wetu utainuka", amesema Bw. Edwin.
‎Kwa upande wake, Bi. Sifa Miyenzi ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo amesema kuwa mwanzoni  mazingira ya biashara sokoni hayakuwa rafiki na hivyo wanatarajia kufanya biashara katika mazingira bora na kuongeza kipato baada ya kukamilika kwa soko jipya.
‎Manispaa ya Iringa inaendelea na utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaotarajiwa kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi ifikapo mwezi Januari, 2027. 

No comments:

Post a Comment