
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Jiji la Dodoma ni miongoni mwa majiji matatu makubwa yanayokuwa kwa kasi kutokana na uwekezaji unaofanywa na Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mhe. Anthony Mavunde, Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Mtumba, ameyasema hayo hivi karibuni wakati akizindua duka la vifaa vya michezo, la Smart Sports linalomilikiwa na mdau wa michezo Bw. George Wakuganda.
Mhe. Mavunde amesema jiji la Dodoma linashughuli nyingi sasa, ikiwemo ya Serikali kuhamia Dodoma ikitokea kwenye Jiji la Dar es Salaam, pamoja na Wizara na baadhi ya taasisi zake kuwepo hapa.

Amesema sasa Dodoma ni kila kitu kwa sasa, na uwepo wa duka hili la vifaa vya michezo ni muhimu na itasaidia kuchochea ukuaji wa michezo hususan mpira wa miguu.
Hatahivyo, amewataka wadau wa michezo kumuunga mkono watu wenye nia njema kwa kupata mahitaji ya vifaa mbalimbali kutokana na kusogezwa karibu kwa vifaa vya michezo, ikiwa ni tofauti na miaka ya nyuma, ilikuwa ni lazima vifaa vifuatwe Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Bw. Alquine Masubo, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) na Kamati ya Mei Mosi Taifa 2026 amesema bila kuwa na vifaa bora hakuna michezo madhubuti, ambapo sasa Kampuni ya Smart Sports imeonesha nia njema ya kushirikiana na wadau wa michezo mahala pa kazi, na baadhi yao kuingia nao mikataba na utoaji wa vifaa vipindi vya mashindano.
“Hata sisi Smart Sports imetudhamini sana kwenye mikutano, mashindano na hata sasa watadhamini michezo ya Mei Mosi inayofanyika mkoani Njombe baadaye mwezi Aprili, 2026, basi tumuunge mkono kwa umoja wetu, ili tukamilishe dhamira yetu ya michezo huku tukitekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Bw. Masubo.
Naye Dkt. Jonas Tiboroha, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Mandeleo ya Michezo Malya; amesema duka hili litakuwa mkombozi kwa wadau wa michezo kwa kununua vifaa vya michezo, ambapo mmiliki wa duka hili amekuwa akiweka michezo mbele zaidi ya fedha, ikiwa ni kuchukua vifaa na kulipa baadaye.
Naye Bw. Wakuganda amesema ushindi katika mashindano mbalimbali unatokana na posho, uvaaji bora wa nguo za michezo na kulala sehemu nzuri, ambapo ametoa wito kwa wadau kushirikiana naye katika ununuaji wa vifaa bora.





No comments:
Post a Comment